Na. Mwandishi Wetu - Dodoma
Serikali
imeahidi kuendelea kusimamia na kulinda haki za Watu wenye Ulemavu nchini ili
kuwezesha kundi hilo kuwa na ustawi mzuri katika nyanja mbalimbali.
Kauli hiyo
imetolewa Februari 25, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi
wakati akifunga Kikao cha Kurekebisha Mpango Kazi wa Taifa kwa Watu Wenye
Ualbino 2022/2023 - 2026/2027 (National Action Plan for Persons with Albinisms
- NAP) kilichofanyika Dodoma Hotel, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri
Katambi alieleza kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na wadau
wanaotoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu ili kuhakikisha utekelezaji wa Sera,
Sheria, Miongozo na Mikataba ya Kimataifa ambapo utekelezaji wake utasaidia
jamii kutambua haki na wajibu wa Watu wenye Ulemavu.
“Kwa muda mrefu
kundi la Watu wenye Ualbino limekuwa katika wakati mgumu wa kufanyiwa vitendo
vya kikatili ambavyo vilichangia kuzorota kwa maendeleo yao ya kijamii na
kiuchumi, hivyo kuandaliwa kwa mpango huu utasaidia kuweka mikakati endelevu ya
utekelezaji wa changamoto zote ambazo wamekuwa wakikabliana nazo,”
“Mpango Kazi
huu wa Taifa kwa Watu wenye Ualbino ni faraja kubwa sana kwetu sisi kama
Serikali pamoja na wadau kwa sababu mpango huu umeweka bayana maeneo makuu
manne ambayo ni ulinzi, uzuaiji, usawa, ubaguzi na uwajibikaji,” alisema Mhe.
Katambi.
Aliongeza kuwa,
Serikali inaendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya kwa Watu wenye
Ulemavu, kuboresha miundombinu ili kujenga mazingira fikivu yatakayo wawezesha
Watu wenye Ulemavu kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki kama watu
wengine.
“Serikali
inatekeleza miradi mbalimbali na katika ujenzi wa miradi hiyo inazingatia
miundo mbinu rafiki kwa Watu wenye Ulemavu ili wawezesha kupata huduma kama
watu wengine na wamekuwa wakipewa kipaumbele wanapoenda kupata matibabu au
huduma nyingine za kijamii mahali popote,” alieleza
Vilevile
alibainisha kwamba Watu wenye Ulemavu wana haki ya kushiriki katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi ikiwemo fursa za ajira au fursa mbalimbali
zinazojitokeza ili wajikwamue kiuchumi badala ya kuendelea kuwa tegemezi, hivyo
alihasa jamii kutambua mchango wa Watu wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya familia
hadi Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Mussa Kabimba
alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kushirikiana na chama hicho cha TAS
pamoja na wadau katika uaandaji wa mchakato huo hadi kufikia hatua ya
kukamilika kwake.
“Tunashukru
watalamu wote kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kitengo cha huduma kwa Watu
Wenye Ulemavu na Idara ya Sera na Mipango kwa namna walivyojitoa kushirikiana
pamoja na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) katika kurekebisha Mpango
kazi huu wa Taifa kwa Watu wenye Ualbino,” alisema
Pamoja na hayo,
alitumia fursa hiyo kupongeza mchakato wa Serikali wa ujenzi wa Vyuo vipya vya
Ufundi Stadi kwa Watu wenye ulemavu katika mkoa wa Kigoma na Songwe sambamba na
maboresha ya vyuo sita vya Ufundi Stadi kwa watu wenye ulemavu ambavyo ni Yombo
- Dar es salaam, Mtapika - Mtwara, Sabasaba - Singida, Luanzari - Tabora,
Masiwani – Tanga na Milongo kilichopo Jijini Mwanza.
Naye Makamu
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Tungi
Mwanjara alihimiza Serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu
kuhusu haki za Watu wenye Ulemavu ili kuhakikisha usalama wa kundi hilo.
MWISHO
Comments
Post a Comment