HALMASHAURI TOENI FEDHA KUTEKELEZA AFUA ZA LISHE- RC MKIRIKITI

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti amezionya halmashauri za mkoa huo kwa kutokutoa fedha za utekelezaji wa afua za lishe katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyekaa katikati) akiwa na Wakuu za Wilaya Sumbawanga Sebastian Waryuba (kulia) pamoja na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Dkt. Boniface Kasululu (kushoto). Waliosimama kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali mara baada ya kikao cha tathmini ya lishe mkoa


Ametoa onyo hilo jana (25.02.2022) wakati akiongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa shughuli za lishe kipindi cha Julai hadi Desemba 2012 kilichofanyika mjini Sumbawanga ambapo halmashauri zote nne ziliripotiwa kutoa fedha za lishe asilimia 17.5 tu hatua inayokwamisha shughuli za lishe.

“Leo ndio siku ya mwisho nisisikie kuwa Afisa Lishe anasema hajapewa fedha za kutekeleza shughuli wakati mkoa bado una tatizo la udumavu na utapiamlo. Wakurugenzi nendeni mkabadilike. Suala la lishe ni agenda muhimu kwa uhai wa watu wetu” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Bonoface Kasululu ilionyesha kuwa halmashauri za Sumbawanga Manispaa, Sumbawanga Vijijini, Nkasi na Kalambo zimetoa asilimia 17 na kupelekea mkoa uwe kwenye rangi nyekundu.

Dkt. Kasululu aliongeza kusema matokeo ya ujumla yanaonesha kuwa mkoa wa Rukwa una wastani wa alama asilimia 87 ambapo kiasi hicho kimechangiwa na kutokutolewa kwa fedha za afua za lishe kwa upande wa halmashauri.

Sehemu ya Maafisa Lishe wa Halmashauri wakiwa kwenye kikao cha tathmini ambapo walieleza kutopata fedha kutekeleza afua za lishe kutoka halmashauri  kipindi cha Julai hadi Desemba 2021


“Asilimia ya bajeti ya halmashauri iliyotumika kutekeleza shughuli za lishe kati ya iliyotengwa rangi nyekundu ni asilimia 17.5 kiashiria hiki kinaendelea kufanya vibaya zaidi ikilinganishwa na matokeo ya asilimia 54 kipidi cha mwaka 2020/2021” alieleza Dkt. Kasululu.

Taarifa ya tathmini kwa kiashiria cha asilimia ya fedha zilizotumika kwa shughuli za lishe katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021 kwenye halmashauri na asilimia zake kwenye mabano Manispaa ya Sumbawanga (0.0), Sumbawanga DC (18.9), Nkasi DC (0.0) na Kalambo DC (47.7) hatua inayofanya mkoa kuwa na jumla ya asilimia 17.5

Mmoja wa Maafisa Lishe toka Halmashauri ambaye hatuka jina litajwe alisema “tumekuwa tukiandika madokezo kuomba fedha za shughuli za lishe lakini hatupatiwi bila kupewa sababu. Oktoba –Desemba, 2021 niliomba shilingi 800,000 lakini hadi leo sijajibiwa na kazi zimesimama” alisema mtaalam huyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) Aron Isaack alisema licha ya mkoa wa Rukwa kushika nafasi ya 13 kati 26 mwaka 2020/21 bado kuna changamoto kubwa ya shughuli za lishe kutopewa kipaumbele hatua inayosababisha utapiamlo na udumavu kuendelea.

Isaack aliongeza kuwa kunahitajika utashi wa kisiasa ili kutekelezwa kwa mkataba wa lishe miongoni mwa viongozi na watendaji wa serikali wakiwemo Waganga Wakuu wa Wilaya za Rukwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kusimamia suala la lishe hasa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 iliyotamka suala la lishe kupewa kipaumbele “alisema Isaack.

Kwa mujibu wa taarifa ya lishe iliyotolewa na Wizara ya Kilimo Desemba 2020 ilionesha kuwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mazao ya chakula ndio ina kiwango kikubwa cha udumavu unaotokana na utapiamlo ikiwemo Rukwa (47.9), Njombe (53.6) na Iringa (47.1).

Mwisho.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.