Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Jumla ya Watumishi 120 wa Mahakama ya Tanzania
kutoka Makao Makuu Dar es Salaam wamefanya ziara ya kutembelea na kujionea
Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama unaojengwa katika eneo la Tambuka
Reli jijini Dodoma ambapo wameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa majengo hayo
yanayotarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu.
Akizungumza na Watumishi hao waliotembelea Mradi
huo tarehe 29 Januari, 2022, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi
aliwaambia Watumishi hao kujiandaa kisaikolojia kwakuwa wapo mbioni kuhamia
Dodoma.
“Ifikapo mwezi wa 12 mwaka huu ninyi wote mtakuwa
mmehamia katika jengo hili, kwahiyo ni vizuri mkajiandaa kisaikolojia na
kufanya maandalizi mengine ya msingi, kwa mfano najua wengine wana Watoto ambao
wanaenda shule, wengine wana wenza wa kuwaweka sawa kisaikolojia, lakini la
msingi la Mtendaji Mkuu kuwapa fursa kuja kuona ni ili mpate picha ya sehemu
mtakayokuja kufanya kazi,” alisema Bw. Nyimbi.
Aliongeza kuwa Watumishi wote wa Makao Makuu,
Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Masjala kuu wote wanatakiwa kuhamia katika
jengo la Makao Makuu ya Mahakama-Dodoma ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi, Afisa Utumishi
wa Mahakama, Bw. Nkrumah Katagira ameshukuru Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole kwa kuwapa fursa ya kutembelea jengo hilo la Makao
Makuu na kuongeza kuwa wamefurahi sana kupewa nafasi hiyo.
“Kwa niaba ya Watumishi wenzangu, nimshukuru sana
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani kwa niaba ya Mtendaji Mkuu, Watumishi kwakweli
wamefurahi sana kwa hii safari, kwa sababu ni sehemu ya kujiandaa kisaikolojia
kujua wapi tutakuja kukaa na hii imepunguza wasiwasi kwetu baada ya kuona
sehemu ambayo tutakuja kufanyia kazi,” alisema Bw. Katagira.
Pamoja na kutembelea Mradi wa ujenzi wa Makao
Makuu, Watumishi hao pia walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma
(IJC) na kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere
‘square’ Dodoma.
Safari hii imejumuisha Watumishi wa Kada za
Wasaidizi wa Kumbukumbu, Wasaidizi wa Ofisi, Wasaidizi wa Maktaba, Makatibu
Mahsusi, Walinzi, Madereva wakiongozwa na Maafisa Utumishi.
Comments
Post a Comment