Na: Mwandishi
Maalum
30/01/2022 Wataalam
wa afya 60 wanaofanya kazi katika hospitali za wilaya na hospitali binafsi za
Mkoa wa Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo ya kutambua moyo unaofanya kazi chini
ya asilimia 50.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akitoa elimu ya jinsi ya kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilimia 50 kwa wataalam wa afya kutoka hospitali za wilaya na binafsi za Mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki mafunzo maalum ya siku mbili ya jinsi ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa yaliyoandaliwa na kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura na kufanyika katika ukumbi wa JKCI leo Jijini Dar es Salaam
Elimu hiyo
imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.
Mohamed Janabi wakati wa mafunzo maalum ya siku mbili ya jinsi ya kutoa huduma
ya dharura kwa wagonjwa yaliyoandaliwa na kituo cha mafunzo cha tiba na huduma
za dharura na kufanyika katika ukumbi wa JKCI leo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika mafunzo hayo Prof. Janabi ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo amesema kuwa JKCI iliona ni muhimu kwa wataalamu hao wa afya kupata elimu
ya kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilima 50 kwani wengi wao wametoka
katika hospitali za wilaya ambazo wagonjwa huanzia huko.
“Tumetoa elimu ya
kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilimia 50 kwa wataalam wa afya wanaoshiriki
mafunzo ya jinsi ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa kwani hawa ndio
wataalam wanaokutana na wagonjwa wengi katika ngazi ya kwanza hivyo kupitia
elimu niliyoitoa itawasaidia zaidi kutoa huduma bora za matibabu wanapokutana
na wagonjwa wa moyo lakini pia kutambua ni kwa wakati gani wanapaswa kuwapa
rufaa wagonjwa hao kufika katika taasisi yetu”, alisema Prof. Janabi
Akizungumzia mafunzo
ya dharura kwa wagonjwa Prof Janabi amesema kuwa wataalam wa afya wanaopata
mafunzo hayo itawasaidia kutoa huduma ya dharura iliyo sahihi kwani hatua ya
kwanza kufanyiwa mtu anayehitaji huduma ya dharura ni ya muhimu kama itafanywa
kwa usahihi hivyo kuokoa maisha ya mgonjwa.
“Kupata ujuzi wa
jinsi ya kutoa huduma ya kwanza haimtaki mtu kuwa daktari tu bali kila mtu
anapaswa kuwa na ufahamu wa kutoa huduma hiyo kwani kwa kuwa na ujuzi huo humsaidia
mtu kuokoa maisha ya mtu mwingine anayehitaji huduma ya dharura mahali popote
pale tatizo linapojitokeza”,
“Iliwahi kunikuta
mara mbili nikiwa katika safari tofauti nimeweza kuokoa maisha wa watu wawili
waliohitaji huduma ya dharura hivyo kuokoa maisha yao, ndio maana nasisitiza
watu wote tuwe na ufahamu wa namna ya kutoa huduma ya dharura kwani dharura
hizo hazitokei hospitali peke yake”, alisema Prof. Janabi.
Kwa upande wake
mkufunzi kutoka kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura Dkt. Silvester
Faya amesema kuwa wameamua kufanya mafunzo hayo kwa ajili ya kuongeza utaalam
kwa watumishi wa afya ili watumishi hao wanapomaliza mafunzo hayo wakabadilishe
maono katika kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa.
Aidha Dkt. Faya
amesema kuwa elimu ya huduma ya dharura bado haijaenea kwa watu ambao sio
wataalam wa afya lakini kupitia wataalam wa afya elimu hiyo inaweza kusogea na
kuwafikia wananchi wengine ili mtu anapohitaji huduma ya dharura aipate pale
shida ilipompata kabla ya kufikishwa hospitalini.
“Tunaamini yakuwa
kama kila mwananchi atapata elimu ya namna ya kumhudumia mtu anayehitaji huduma
ya dharura tutapunguza madhara mengi yayaoweza kumpata mgonjwa ikiwemo
kupunguza vifo vinavyotokana na kukosa huduma ya dharura kwa wakati” alisema
Dkt. Faya
Akizungumzia
mafunzo hayo Mratibu wa huduma za dharura Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Paschal
Mgaya amesema kuwa nafasi waliyoipata madaktari na wauguzi wachache kutoka
katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam iwe chachu kwa watoa huduma
wa afya wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo.
“Mafunzo haya
yatatusaidia zaidi katika mkoa wetu wa Dar es Salaam kwani wale wachache
waliopata mafunzo haya wataenda kutoa elimu hiyo kwa wataalam wengine ambao
hawakupata nafasi ya kushiriki hivyo kupunguza changamoto nyingi zilizopo
katika kutoa huduma ya dharura na kuokoa maisha ya wagonjwa”, alisema Dkt.
Mgaya.
Naye afisa
Muuguzi kutoka hospitali binafsi ya Sali Judithi Kashe amesema kuwa kupitia
mafunzo maalum ya jinsi ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa amepata nafasi
ya kujifunza vitu vingi vipya ambavyo hakuwa anavijua hivyo mafunzo hayo kwenda
kuongeza tija katika utendaji kazi wake wa kila siku.
“Mafunzo
tuliyoyapata leo hii yametujenga wataala wa afya kutoa huduma inayofanana na ya
usahihi kwa wagonjwa wetu kwani watu wengi hupoiteza maisha pale mwanzoni
wanapokosa huduma sahihi ya dharura”, alisema Judith
Comments
Post a Comment