POSTA YATAKIWA KUTUMIA ANWANI ZA MAKAZI KUBUNI HUDUMA MPYA KWA WATEJA

 


Prisca Ulomi na Loema Joseph, Dodoma

Serikali imelitaka Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutumia mfumo wa anwani za makazi na postikodi kubuni huduma mpya kwa wateja ili utekelezaji wa mfumo huo utakapokamilika uweze kutumika ipasavyo kufikisha huduma na bidhaa kwa wateja

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Teddy Njau wakati akifungua semina ya mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwa Mameneja wa Mikoa ya Shirika hilo wa Tanzania Bara na Zanzibar

Njau amewataka washiriki hao kuweka anwani za makazi kwenye maeneo yao; kwa wateja wao na kubuni huduma mpya zitakazotumiwa na wateja kupitia mfumo wa anwani za makazi utakapokamilika utekelezaji wake kwa kuwa Shirika hilo lina mtandao mpana nchi zima na ni wadau wa msingi wanaotakiwa kutumia miundombinu hiyo

“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anwani za makazi zinawekwa na kutumika nchi nzima, leo mnapatiwa mafunzo ya kujenga uelewa ili mkasimamie na kushiriki utekelezaji wa mfumo huu kwenye mikoa yenu Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa ninyi ni wadau muhimu na ni wajumbe kwenye kamati za kitaalam,” amesisitiza Njau

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Caroline Kanuti amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi utakuwa wa kidijitali ili kutoa fursa kwa Serikali kutekeleza majukumu ya sensa ya watu na makazi ili anwani zijumuishwe kwenye sensa inayoanza mwezi Agosti mwaka huu

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi utafanyika kwa miezi mitano nchi nzima kwenye kata na wadi 4,174; halmashauri 196 na mikoa 31 ili zoezi hili likamilike ipasavyo na taarifa zake ziwekwe kwenye tovuti maalum na zitumike kwenye simu za mkononi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo amesema kuwa Shirika lake ni mdau muhimu katika anwani za makazi na postikodi ndani na nje ya nchi kwa kuwa posta zote duniani zina jukumu la kutoa anwani zinazotambulika na muundombinu huu utakapokamilika Shirika litatumia anwani za makazi kusafirisha huduma na bidhaa kwa wananchi mpaka nyumbani kwa kuwa tayari tuna duka mtandao

“Mwananchi anaweza kununua na kuuza huduma au bidhaa na kuweka anwani yake kisha atasafirishiwa mzigo wake mpaka mahali alipo na mwananchi atatumia muda wake kutekeleza majukumu mengine ya kiuchumi na kijamii badala ya kufuata mzigo wake, tutashirikiana na viongozi na wataalam wengine nchi nzima kutekeleza hili,” amesema Mbodo

Amesititiza kuwa Shirika lina duka mtandao ambalo linamuwezesha mwananchi wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara mtandao na kutumia huduma za Shirika hilo kwa kuwa limeunganishwa na mtandao wa ofisi nyingine za Posta 670 duniani zilizopo kwenye nchi 192 wanachama wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) ambapo Tanzania ni nchi mwanachama.

Mwisho.






Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.