Na WMNN, Dar es Salaam
KUTOKANA
na mauaji ya kijamii yanayoendelea nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni amepanga kukutana na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi
ili kujadili jinsi ya kudhibiti mauaji hayo.
Waziri
Masauni amesema katika kikao hicho pia kitajadili jinsi ya kulifanya Jeshi la
Polisi kuwa la kisasa katika kudhibiti matukio mbalimbali kiuhalifu nchini.
Akizungumza
katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea Kamisheni ya Uchunguzi wa
Kisayansi (Forensic Bureua), jijini Dar es Salaam, leo, Masauni amesema lengo
kuu la kukutana na viongozi hao siku ya Jumatatu Januari 31, 2022, ni kupata
taarifa ya uchunguzi wa mauaji ambayo waliushaanza na kujua jinsi gani matukio
hayo yanaweza kumalizwa katika jamii.
“Siku
ya Jumatatu nitakua na kikao na Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na IGP
pale Wizarani kwa ajili ya kupitia matokeo ya kazi ya uchunguzi ambayo
wanaifanya na Serikali tunategemea waifanye ili tuweze kuwajulisha wananchi juu
ya hayo matukio yote ili tujue tulipofikia, hatua zake ni zipi, na mafanikio
yake ni yapi na mikakati kuweza kuhakikisha mambo kama haya ya mauaji tunaweza
tukayapunguza katika siku za usoni,” alisema Masauni.
Waziri
Masauni aliongeza kuwa, lengo kuu la ziara yake ni kutaka kuona Kamisheni hiyo
ya Uchunguzi jinsi inavyochunguza na kudhibiti mauaji pamoja na kuhakikisha
wahalifu wanapatikana kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Aidha,
Masauni alizungumzia kuhusu uhalifu wa kimtandao ambapo aliliagiza Jeshi la
Polisi kuwasaka wanaosajilia watu laini za simu, wanaochafua viongozi na wanaosambaza
picha chafu mitandaoni.
Alisema suala la uhalifu wa kimtandao limekuwa
kubwa katika siku hizi za karibuni na kadiri siku zinavyokwenda mbele na
teknolojia inavyozidi kutanuka ndipo matatizo ya uhalifu wa kimtandao
yanavyoongezeka, hivyo ni lazima Jeshi liwe tayari kukabiliana na mabadiliko ya
aina yoyote katika kudhibiti uhalifu huo ambao haukubaliki na hauwezi kuachwa
uendelee.
“Wapo
watu wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kudhalilisha watu wengine, wengine ni
watu wazima wanaweza kuwa hata wazazi wao, wapo wanaotumia mitandao kufanya
wizi na uitapeli kwa raia wengine, wapo watu ambao wanajadili mambo ambayo yapo
kinyume na maadili, desturi za watanzania, ambapo haya yote yanayoendelea
kufanyika lazima yadhibitiwe na Jeshi la Polisi, kwahiyo kuna haya ya
kuhakikisha haya yote yanafanyika kwa kasi zaidi,” alisema Masauni.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu wa Kimtandao, SSP Joshua Mwangasa,
alimshukuru Waziri huyo kwa kutembelea Kamisheni hiyo na kuahidi kutekeleza
maelekezo yote aliyoyatoa.
“namuahidi
Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla hili suala tutalifanyia kazi usiku na
mchana, amejionea mwenyewe jinsi tunavyofanya kazi na jinsi gani tunavyopambana
na uhalifu wa kimtandao, kwahiyo cha msingi ni kupokea maelekezo na kuyafanyia
kazi ili changamoto nyingi sana tuweze kuzifanyia kazi na kuzimaliza,” alisema SSP Mwangasa.
Waziri
Masauni alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoimarisha vyombo
vya ulinzi na usalama nchini vikiwemo vyombo vilivyopo ndani ya Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi vimeweza kujengewa mazingira mazuri katika kipindi cha uongozi
wake kwenye eneo la stahiki na maslahi ya askari wetu kwenye eneo la
kupandishwa vyeo, kupunguza changamoto ya ajira kwa kuajiri vijana wapya na
kuwapa vifaa vya kisasa vinavyoweza kuweza kufanya kazi ambazo ameziona katika
ziara yake katika Kamisheni hiyo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment