DKT. MOLLEL AHIMIZA USHIRIKISHAJI WA WAKUU WA MIKOA /WILAYA KATIKA MAPAMBANO YA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin
Mollel ,amezindua mpango endelevu wa kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele na mpango mkakati wa mwaka 2021/2026 wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti
magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Mpango wa kudhibiti magonjwa
yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ulianza mwaka 2009 kwa kuunganisha miradi ya
magonjwa matano ambayo ni trakoma, usubi, matende na mabusha na kudhibiti
kichocho na minyoo ya tumbo ili kurahisisha utekelezaji wake.
Akizindua mpango huo jana jijini Dodoma, Dkt Mollel
amehimiza ushirikishwaji wa wakuu wa mikoa na wilaya katika mapambano ya
kutokomeza ugonjwa ili kufikia lengo liliopo la kuumaliza kabisa ifikapo mwaka
2030.
‘’Magonjwa haya yalikuwa yana
athiri wilaya 119 nchi nzima .Lakini leo tuna wilaya nane tu ambazo bado zinaathiriwa
na hili tatizo ‘’ amesema Dkt. Mollel
Wakati huo huo , amesema pamoja
na kwamba wataalam kufanya kazi nzuri katika mapambano hayo bado kuna nafasi ya
kuendelea kupambana na magonjwa hayo.
‘’Umesikia Rais Samia ametoa
zaidi ya bilioni 18 maana yake ni kwamba serikali imewekeza sana kwenye
kuumaliza hili tatizo’’ ameongeza Dkt. Mollel
Akizungumzia kwa upande wa
magonjwa ya mabusha na matende, Mkuu wa wilaya Dodoma Jabir Shekimwei, amesema katika miaka mitano
iliyopita wamejitahidi kutokomeza changamoto ya tatizo hilo
Kwa upande wake Dkt. Azma Simba Mwakilishi wa Mkurugenzi wa
Huduma za Kinga kutoka wizara ya afya ,amesema kulingana na taarifa za
tathimini mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa watanzania wapo katika
hatari ya kupata magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele hususan minyoo
ya tumbo na kichocho.
‘’Watanzania milioni 65 wako
katika hatari ya kupata magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele hususan minyoo
ya tumbo na kichocho’’ amesema Azma
Maadhimisho ya mwaka huu yana
kwenda sambamba na kauli mbiu isemayo Usawa na Uwiano wa utoaji huduma za afya
ili kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Lengo la kauli mbiu hiyo ni kukumbusha magonjwa hayo kupewa nafasi
inayostahili katika huduma au mifumo ya kutolea huduma za afya.
Comments
Post a Comment