Bodi
ya Nishati Vijijini inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imehitimisha
muda wake kisheria na kupongezwa kwa kutekeleza majukumu yake kwa juhudi,
weledi, uadilifu na uzalendo.
Akizungumza
mwishoni mwa juma, katika hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa Bodi hiyo, Mgeni
Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali aliwaeleza kuwa
Serikali inatambua mchango wao katika majukumu mbalimbali waliyotekeleza,
hususani katika kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini hadi kufikia
asilimia 69.8.
Mahimbali
ambaye alimwakilisha Waziri wa Nishati, alieleza majukumu mengine
yaliyotekelezwa na Bodi hiyo kwa ufanisi mkubwa ni pamoja na kuongezeka
uunganishaji umeme kwa wateja wa vijijini kutoka 584,639 hadi kufikia wateja
956,511 sawa na asilimia 63.6.
Alitaja
mafanikio mengine kuwa ni kusimamia kuongezeka kwa Mfuko wa Nishati Vijijini
kutoka Shilingi Bilioni 1,337 hadi Bilioni 1,684 sawa na asilimia 26. Aidha,
kuongezeka kwa michango ya wabia wa maendeleo kutoka Shilingi Bilioni 252 hadi
Bilioni 560 sawa na asilimia 123 pamoja na kusimamia kikamilifu maslahi ya
wafanyakazi wa Wakala.
Naibu
Katibu Mkuu alieleza zaidi kuwa, Bodi ilisimamia kikamilifu utekelezaji wa
jukumu la msingi la Wakala ambalo ni kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa
nishati bora vijijini ili kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini,
kiuchumi na kijamii kupitia upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo kuifanya
Serikali kutembea kifua mbele kwa mafanikio yaliyopatikana ambayo yameacha
alama Tanzania na Afrika nzima.
“Kwa
niaba ya Serikali, ninawashukuru kwa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Nishati
Vijijini kwa uadilifu mkubwa na maslahi mapana ya Taifa. Kwa hakika, kazi hii
ni ngumu na inahitaji watu wenye uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kutekeleza
majukumu haya kama mlivyofanya ninyi.”
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo, alitoa shukrani kwa
Serikali, Wabia wa Maendeleo, Wizara ya Nishati, Menejimenti na Wafanyakazi
wote wa REA, kwa ushirikiano wa hali na mali katika kuiwezesha Bodi kutekeleza
majukumu yake kikamilifu.
Wakili
Kalolo alifafanua kuwa, kitendo cha Serikali na Wabia wa Maendeleo kuendelea
kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati vijijini
kimeiwezesha Bodi hiyo kupata mafanikio yote iliyofikia.
Aidha,
alisema kuwa ushirikiano uliotolewa na wafanyakazi wote wa REA, Wizara na
Taasisi mbalimbali zinazohusiana na Wakala huo, umechangia kwa kiasi kikubwa
kufikia mafanikio hayo.
Akitoa
salamu za shukrani kwa niaba ya Wajumbe wenzake wa Bodi, Mkurugenzi Dailin
Mghweno alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaamini na
kuendelea kuwapa nafasi ya kuwatumikia Watanzania hadi walipohitimisha muda
wao.
Naye
Mkurugenzi Mhandisi Francis Songela aliahidi kuwa Wajumbe wote wa Bodi hiyo
wataendelea kutoa ushirikiano kwa REA na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha
malengo yote yaliyopangwa kutekelezwa yanafikiwa.
“Tutaendelea
kuwa Mabalozi wazuri na tuko tayari muda wote kutoa ushirikiano pale
utakapohitajika,” alisisitiza Mhandisi Songela.
Katika
hafla hiyo, Mgeni Rasmi aliwatunuku tuzo na vyeti maalum kama ishara ya
kutambua utumishi wao uliotukuka ambao umeleta tija katika sekta ya nishati
vijijini.
Wajumbe
wa Bodi hiyo iliyoteuliwa Januari 31, 2019 na ambayo imehitimisha muda wake wa
miaka mitatu kisheria ni Mhandisi Styden Rwebangila akiwakilisha Wizara ya
Nishati, Dailin Mgweno (Umoja wa Walaji Tanzania), Mhandisi Francis Songela
(Wabia wa Maendeleo), Louis Accaro (Sekta Binafsi), Frolian Haule (Vyama vya
Ushirika) na CPA Oswald Urassa (Umoja wa Benki Tanzania).
Comments
Post a Comment