Na Rayson Mwaisemba
WAMJW-DODOMA.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Bodi ya Maabara Binafsi imeendelea kutoa
mafunzo kwa Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Halmashauri ili kuwajengea
uwezo juu ya namna bora ya kusimamia na kuboresha huduma zinazotolewa na
Maabara Binafsi za Afya nchini.
Mafunzo hayo ya siku tatu
yanayoendelea Jijini Dodoma yamefunguliwa leo na Msajili wa Maabara Binafsi za
afya kutoka Wizara ya Afya Bw. Dominic Fwiling’afu aliyemwakilisha Mganga Mkuu
wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe.
Katika mafunzo hayo Msajili wa
Maabara Binafsi Bw. Dominic Fwiling’afu amesema, katika utoaji wa huduma za
afya kwa wananchi, mnamo mwaka 1997 Serikali ilipitisha Sheria Sura 136 ya
kusimamia utoaji wa huduma za Maabara Binafsi za Afya Lengo ni kuhakikisha
huduma zinatolewa na maabara binafsi za afya zinakidhi vigezo na kuzingatia
viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Katika jitihada za kuimarisha
upatikanaji na utoaji huduma za afya kwa wananchi, mnamo mwaka 1997 Serikali
ilipitisha Sheria Sura 136 ya kusimamia utoaji wa huduma za Maabara Binafsi za
Afya ili kuhakikisha huduma zinatolewa na maabara binafsi za afya nchini
zinakidhi vigezo na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.” Amesema.
Amesema, katika mafunzo haya
waratibu watapata fursa ya kupitishwa kwenye changamoto mbalimbali
zilizobainika kwenye kaguzi zilizofanywa na Bodi kwenye Mikoa mbalimbali na
kuweka mikakati ya pamoja ya kuweza kuzitatua changamoto hizo ili kuboresha
utekelezaji wa majukumu ya Bodi.
Aidha, Bw. Fwiling’afu amesema
kuwa, mafanikio yatakayopatikana baada ya kikao hiki yatasaidia kwa kiasi
kikubwa utoaji wa huduma bora za Afya nchini, kwani huduma hizi zina umuhimu wa
pekee katika kutambua vyanzo vya magonjwa na matibabu yake kisayansi.
”Mafanikio yatakayopatikana
baada ya kikao hiki ni wazi kuwa yatachangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma
bora za Afya nchini, ikizingatiwa kuwa, huduma za maabara zina umuhimu wa pekee
katika kutambua vyanzo vya magonjwa na matibabu yake.” Amesema.
Mafunzo haya yanayotolewa na
Bodi yakawe chachu kwenu kuhakikisha maabara binafsi zote mnazosimamia zinatoa
huduma zenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, kwa kuzingatia
Sheria, Kanuni na miongozo yote inayotolewa na wizara ya Afya inayohusu uanzishwaji
na usimamiaji wa huduma bora za Maabara Binafsi za Afya ili wagonjwa wapate
tiba sahihi na kwa wakati, amesisitizi Bw. Fwiling’afu.
Mbali na hayo, ameweka wazi
kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuona mabadiriko makubwa baada
ya mafunzo haya ikiwemo kutumia wataalamu wenye sifa na kuzingazia kanuni na
miongozo ya utoaji wa huduma, Maabara Binafsi za Afya zote nchini kusajiliwa na
Bodi ya Maabara Binafsi za Afya, kulipa ada za mwaka kwa wakati, Maabara
binafsi za afya zote zinaorodheshwa kwenye mfumo wa usajili wa vituo (HFRS) ili
Kuimarisha utunzaji na upatikanaji wa taarifa.
Nae, Mkuu wa Kitengo cha Huduma
za dawa OR. TAMISEMI Bw. Mathew Mganga ametoa wito kwa Waratibu wa Maabara wa
Halmashauri zote nchini kuwa kichocheo cha kukuza taaluma ya huduma za maabara
ili wananchi wapate huduma bora na kwa wakati, hali itayoijengea taswira nzuri
Serikali inayosimamia huduma hizo.
Pia, amewataka Wataalamu hao
kusimamia utoaji huduma za maabara kwa kufuata kanuni, miongozo, taratibu na
Sheria za utoaji huduma za maabara bila kumwonea mtu ili kuondoa kero na
malalamiko kuhusu huduma kutoka kwa wananchi.
Mwisho.
Comments
Post a Comment