Na Munir
Shemweta, WANMM TARIME
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekagua uimarishaji
mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Kenya katika eneo la hifadhi ya Taifa
ya Serengeti mkoani Mara na kupongeza wapima wa nchi hizo mbili kwa
kufanikisha kuweka alama 205.
Aidha,
Waziri Lukuvi aliwashukuru marais wa Tanzania na Kenya kwa kukubaliana
kuendelea na kazi ya uimarishaji mpaka huo wa kimataifa kwenye eneo la hifadhi
ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti na Masai Mara kwa upande wa Kenya ambapo
uimarishaji wake ulisimama kwa muda.
‘’Kwa
muda mfupi timu za nchi hizo mbili zimeweza kuweka alama 205 katika eneo hili,
kazi ilianza 2018 tulipofika eneo la hifadhi tulisiamama kidogo na
uendelezaji huu unaofanyika umechangiwa na ziara ya Rais Samia
Suluhu Hassan kule nchini Kenya kuzungumza na mwenzake Uhuru Kenyata na
kukubaliana na ndiyo maana wapima wamendelea na kazi hiyo’’ . alisema Lukuvi
Akiwa
katika eneo la Serengeti tarehe 21 Desemba 2021 katika ziara ya kukagua
uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya, Waziri Lukuvi
alisema, anaamini sasa nchi hizo mbili zinaenda kumaliza kuweka alama kwenye
mpaka mzima unaofikia kilomita 758 ambapo kwa sasa zimefikiwa kilomita 232 na
kuahidi zote kumalizwa.
Akigeukia
kuhusu eneo la ukingo wa mpaka (Buffer Zone) Waziri Lukuvi alisema, kwa sasa ni
vyema utengenezaji barabara ukazingatia eneo la mita tano aliyoieleza kuwa ni
muafaka wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, mazungumzo bado yanaendelea
kuona kama ipo haja ya eneo hilo kuongezwa.
‘’Serikali
itaendelea kusaidia ili kazi hii ya uimarishaji mipaka ya Kimataifa iende
vizuri na uwekaji alama hizi siyo uadui bali ni kuwa na mipaka inayoonekana
itkayoondoa hofu. Kama mtu akitaka kufanya uovu asisingizie kama hajui mpaka na
alama tutaweka kote hata majini’’. Alisema Lukuvi.
Mkurugenzi
wa Upimani na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny
Mansour .alisema, kazi mbalimbali zimefanyika wakati wa uimarishaji mpaka mpaka
huo zikiwemo utoaji elimu, kuanisha sehemu ya kujenga, kujenga alama za mpaka
pamoja na kukusanya taarifa za kijiografia.
Mpima
kutoka Idara ya Upimaji nchini Kenya Ibrayan Sabwa alieleza kuwa,
katika kipindi chote cha kazi ya uimarishaji mpaka eneo la hifadhi ya
Taifa ya Serengeti na ile ya Masai Mara kwa upande wa Kenya wamekuwa na
ushirikiano mzuri baina ya timu za nchi hizo na kubainisha kuwa na hakukuwa na
shida yoyote wakati wa kazi hiyo.
‘’Tumekuwa
tukiendelea vizuri, na kazi imeenda vizuri sana, watanzania wamekuwa
wakishirikiana na sisi vizuri hawakuwa na shida yoyote na nina imani kazi
itakamilika vizuri. Watanzania ni marafiki zetu na wao ni marafiki zetu’’
alisema Sabwa.
Mapngo
kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhusiana na uimarishaji mipaka wa Tanzania na
Kenya ni kukamilisha awamu ya I ya Km 238 kwa kukamilisha kipande cha
hifadhi cha Km 60 na eneo la Natron la Km 23 pamoja na kuimarisha awamu ya II
yenye jumla ya kilomita 110 ya mpaka kutoka Ziwa Natron hadi Namanga katika
wilaya ya Longido.
Mpaka
wa Tanzania na Kenya una urefu wa nchi kavu wa Km 758 uliowekwa kwa makubaliano
ya wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza mwaka 1893 chini ya mkataba wa
Anglo-Germany Agreement na Protocal kukubalika mwaka 1906.
Comments
Post a Comment