Na. Edward Kondela
Maafisa kutoka Idara ya Mifugo
na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mkoa wa Simiyu na wilaya zake
wametakiwa kuwa na mkakati wa pamoja kuhakikisha zoezi la uwekaji hereni za
kieletrroniki kwa mifugo linafikia malengo yaliyokususdiwa.
Akizungumza hayo (21.12.2021) wakati wa utambulisho wa mwongozo wa utambuzi, usajili na
ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki Mkoani Simiyu, Kaimu
Katibu Tawala wa mkoa huo Mhandisi Mashaka Luhamba amesema zoezi hilo linapaswa
kufanywa kwa umakini mkubwa kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ni kati ya mikoa yenye
idadi kubwa ya mifugo hapa nchini.
Mhandisi Luhamba amefafanua kuwa
uongozi wa mkoa, utahakikisha unafanya ufuatiliaji na kuhitaji taarifa ya mara
kwa mara juu ya utekelezaji wake ili kupata matokeo chanya ya kufahamu idadi ya
mifugo iliyopo Mkoani Simiyu pamoja kuiongezea thamani kwa kutoharibu ngozi za
mifugo kwa kuiwekea alama kwa njia ya moto.
Akielezea juu ya mwongozo wa
utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki
katika mkutano huo, Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema hereni zinawekwa kwa mnyama mwenye umri
zaidi ya miezi mitatu na kwamba zitasaidia pia kupunguza muingilianio wa mifugo
kutoka maeneo mengine.
Pia, amesema zoezi la uwekaji
hereni za kieletroniki kwa mifugo linalofanyika kote nchini litamuwezesha
mfugaji kuweza kupata mikopo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na
kuikatia bima mifugo yake kwa kutumia namba za usajili zilizopo kwenye reheni
ya mnyama.
Kwa upande wake Kaimu Afisa
Mifugo Mkoa wa Simiyu Bw. Juma Kazula, akizungumza wakati wa kuahirishwa kikao
hicho amesema wajumbe wamekubaliana ifikapo Tarehe 15 Mwezi Januari Mwaka 2022
kila halmashauri iwe imeandaa mpango kazi wa utekelezaji wa zoezi la uwekaji
hereni za kieletroniki kwa mifugo na zoezi la uwekaji hereni likamilike Tarehe
15 Mwezi Julai Mwaka 2022 pamoja na uwepo wa taarifa ya kila mwezi juu ya zoezi
hilo, huku Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Itilima Dkt. Kiraba Musoke
akiwaasa wajumbe hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana ili mifugo
mingi iweze kusajiliwa.
Awali maafisa kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi wakiongozwa na Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za
Mifugo wamekutana na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo kwa ajili
ya kuutambulisha mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa
njia ya hereni za kieletroniki katika mkoa huo, ambapo Bi. Kayombo amesema
hereni hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza thamani ya ngozi ya mifugo
ambayo imekuwa ikiharibiwa kwa kuwekewa alama kwenye ngozi kwa njia ya moto.
Zoezi la utambuzi, usajili na
ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki linafanyika kwa mujibu
wa Sheria ya Mwaka 2011 ambapo linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya
Shilingi 1,750/= kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000/= kwa mbuzi na kondoo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment