Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinafanya jitihada
kubwa ili kuwafanya wavuvi wawe na uhakika wa kupata samaki pindi wakienda
majini badala ya kuwinda kama wanavyofanya hivi sasa.
Mhe. Ulega
ameyasema hayo jana (21.12.2021) kwenye hafla ya kuwakabidhi wavuvi vifaa
maalum vitakavyowawezesha kutambua maeneo yenye samaki kabla ya kuingia
majini na kuanza shughuli ya uvuvi iliyofanyika Shehia ya Kizimkazi Mkoa wa
Kusini Unguja (Zanzibar).
“Kwanza
nimefarijika kuona wavuvi wengi kwenye shehia hii ni vijana hivyo nina uhakika
itakuwa rahisi wao kutumia vifaa hivi na kuwafundisha wazee ambao bado
wanaendelea na shughuli za uvuvi kwa hapa Kusini Unguja” Ameongeza Mhe. Ulega
Mhe. Ulega
ameiagiza Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu kutoa mafunzo ya matumizi
sahihi ya vifaa hivyo ili wavuvi hao waanze kuvitumia ambapo ametoa rai kwa
wavuvi kutumia vizuri teknolojia hiyo.
“ Lakini
pia vifaa hivi tunavyogawa leo ni vichache hivyo niwaelekeze mamlaka ya
kusimamia uvuvi wa bahari kuu kuongeza wigo wa usambazaji wa vifaa hivi muhimu
na hatimaye viweze kuenea kwa wavuvi wote waliopo Zanzibar na Tanzania bara”
Ameagiza Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega
ameongeza kuwa hatua ya kugawa vifaa hivyo itaendelea kuchochea kampeni ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya kuhakikisha pande hizo zinaingia kwenye uchumi wa buluu jambo ambalo ameweka
wazi kuwa litainua uchumi wa wavuvi kwa kiasi kikubwa.
Awali
akisoma taarifa ya ulinzi wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa Visiwa vya
Unguja na Pemba Kamanda wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM)
Comodore Azana Msingiri amebainisha kuwa kumekuwa na changamoto ya baadhi
ya wavuvi kutotii sheria bila shuruti ambao huiona mamlaka yake kama kandamizi
pindi wakichukuliwa hatua ambapo amewataka wavuvi kutambua kuwa ulinzi wa
rasilimali za Uvuvi kwa upande wa visiwa hivyo ni jukumu ambalo mamlaka yake
inalitekeleza kisheria.
“Hivi
karibuni kuna tukio moja lilitokea kwa baadhi ya Wavuvi kubishana na KMKM na
mimi nilipopata taarifa ya kutosha kutokana na mzozo huo niliamuru kikosi hicho
kiondoke katika eneo hilo kwa sababu wangeendelea wakati wao wana silaha
ingeweza kutokea hata umwagaji wa damu” Amesema Comodore Msingiri.
Comodore
Msingiri amewaeleza wavuvi waliofika kwenye halfla hiyo kuwa hakuna mtu
yoyote aliyepo juu ya sheria hivyo ni vizuri kufuata maelekezo yote wanayopewa
na mamlaka hiyo ambapo amesisitiza kuwa mamlaka yake imejidhatiti kuhakikisha
inatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Akielezea
kuhusu mapokezi ya Wavuvi kuhusu Vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya
kusimamia Uvuvi wa bahari Kuu Zahor El.Kharousy amesema kuwa tangu
kuanza kutumika kwa vifaa hivyo kiwango cha upatikanaji wa samaki
kimeongezeka ambapo kwa hivi sasa mvuvi mmoja anaweza kupata kiasi cha kilo 38
za samaki kwa saa moja.
“Kuongezeka
kwa kipato kinachotokana na Uvuvi kumewawezesha wavuvi hao kukidhi mahitaji yao
ya kila siku na kufanya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na baadhi yao
kujenga makazi ya kudumu, kuboresha zana za Uvuvi na kusomesha watoto wao”
Amesema El. Kharousy.
Mkurugenzi
huyo ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza jumla ya vifaa 64 vya kusomea maeneo
ya upatikanaji wa samaki na simu za mkononi 21 vyote vikiwa na thamani ya
milioni 200.8 viligawiwa kwa wavuvi hao ambapo amebainisha kuwa fedha zote za
kugharamia vifaa hivyo zimetoka katika mradi wa SwioFish unaotekelezwa kwa
ufadhili wa benki ya Dunia.
Akitoa
shukran kutokana na vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Rashid
Rashid amebainisha kuwa vifaa hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wavuvi waliopo
kwenye mkoa wake ambapo aliwataka wavuvi hao kutumia vifaa hivyo kwa umakini
ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu zaidi.
“Lakini pia
nimemuomba Mhe. Ulega msaada wa majaketi ya kujiokoa na majanga ya majini
ambapo ameahidi kunipatia majaketi hayo hivyo nikushukuru sana Mhe.
Ulega” Amesema Mhe. Rashid.
Mhe. Rashid
ameeleza kuwa mbali na vifaa hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu imetoa jumla ya boti 70 kwa wavuvi
wote wa Mkoa wake ambapo ameongeza kuwa kinachosubiriwa hivi sasa ni kupokea
boti hizo.
“Boti hizi
tutazigawa kwa wavuvi na tayari wenzetu wa uvuvi wa bahari kuu wameshatupa
maelekezo kuhusiana na hilo lakini vile vile Mkoa wetu umepatiwa jumla ya boti
50 za uvuvi wa mwani na muda si mrefu tutapa vifaa vya uvuvi wa kaa na majongoo
hivyo tunamshukuru sana Mhe. Rais wetu wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha Uchumi wa buluu unawezekana” Amehitimisha
Mhe. Rashid.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa
zikifanya jitihada mbalimbali zitakazoziwezesha nchi hizo kuingia kwenye uchumi
utakaotegemea Rasilimali za Uvuvi zilizopo ukanda wa bahari kuu (Uchumi wa
buluu).
Comments
Post a Comment