MPANGO KABAMBE UPELEKAJI NISHATI VIJIJINI WABAINISHWA

Na Veronica Simba  - Kigoma

Imeelezwa kuwa Mpango Kabambe wa Kupeleka Nishati Vijijini umelenga kuwanufaisha wananchi kupitia usambazaji umeme pamoja na nishati bora ya kupikia.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza (kulia) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kushoto) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Jaffary Mpina (wa pili – kushoto)


Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Kigoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy, walisema kuwa Mpango huo unahusisha nishati za aina mbalimbali, siyo umeme peke yake.

Wakili Kalolo alisema kuwa, ni jukumu la REA kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziwasaidie kuboresha maisha yao, hivyo Wakala umejiwekea mikakati ya kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa ipasavyo.

Akifafanua, alisema kuwa REA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na inaendelea kufanya vema katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hivyo hakuna shaka katika utekelezaji wa miradi ya aina nyingine za nishati zilizofanyiwa tafiti, utakuwa wenye ufanisi pia.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza (kulia) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kushoto) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Jaffary Mpina (wa pili – kushoto


Akitoa mfano, alisema kuwa tafiti zinaonesha eneo jingine muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ni katika nishati ya kupikia ambapo asilimia kubwa ya waathirika ni wanawake, ambao kutokana na matumizi ya kuni, wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya macho na kifua.

Alisema, ni kwa sababu hiyo, Wakala umedhamiria kuondoa adha hiyo katika jamii hususani wanawake waishio vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu akidadavua zaidi kuhusu Mpango huo kabambe, alieleza kuwa umejikita katika sehemu mbili kubwa ambazo ni usambazaji umeme pamoja na nishati ya kupikia.

Alieleza zaidi kuwa, hivi sasa, Wakala unaongeza nguvu zaidi katika nishati ya kupikia ili kuhakikisha kwamba wananchi hususan wa vijijini, wanatumia nishati bora kwa shughuli za kupikia na kupunguza au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa ambao upatikanaji wake ni mgumu, aghali na siyo rafiki kwa mazingira.

Mhandisi Saidy alisema REA imefanya tafiti kadhaa za majaribio kuhusu nishati ya kupikia mathalani mradi wa kutumia tungamotaka, ambapo mifumo husika ilipelekwa katika maeneo 725 yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.

Aidha, aliongeza kuwa, Wakala umeshirikiana na kampuni za usambazaji gesi kufanya tafiti kuhusu uwezekano wa kuhakikisha nishati ya gesi inafikishwa katika maeneo ya vijijini kwa gharama nafuu ili wananchi waweze kuitumia kwa shughuli za kupikia.

Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwahakikishia Wakuu wa Wilaya za Kibondo na Kakonko, ambao walikutana nao kwa nyakati tofauti, kuwa maeneo yote ya kimkakati, hasa yanayohusisha masuala ya usalama yatapelekewa huduma ya umeme ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa ufanisi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kulia) wakijadiliana jambo wakati walipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Kibondo kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme


Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Malassa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Kanali Aggrey Magwaza, kwa nyakati tofauti waliomba maeneo ya mpakani ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme, yapewe kipaumbele katika kufikishiwa nishati hiyo ili kuimarisha shughuli za kiusalama.

Pia, Wakuu hao wa Wilaya walipongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Wakala wa Nishati Vijijini katika kusambaza umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu pia walikagua miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kukutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ambapo walijadili changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.

Kupitia kikao hicho, viongozi hao waliipatia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji vifaa iliyokuwa ikimkabili Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Kampuni Tanzu ya TANESCO (ETDCO) katika wilaya za Kakonko na Kibondo.

“Utekelezaji ulikuwa nyuma kidogo kutokana na changamoto ya vifaa. Tumetatua changamoto hiyo na tumemwelekeza Mkandarasi ndani ya miezi mitatu awe amekamilisha mradi huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu.

Aidha, Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo katika wilaya za Buhigwe, Kasulu, Kigoma Vijijini na Uvinza, Kampuni ya M/s CCCE Etern Consortium alielekezwa kuongeza nguvu ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati uliopangwa ambao ni mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba, 2021.

Miradi mingine inayotekelezwa mkoani Kigoma ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kuanza hivi karibuni pamoja na Mradi wa Ujazilizi unaolenga kufikisha umeme katika maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya nishati hiyo lakini umeme haujashushwa.

Katika ziara hiyo, viongozi hao wa REA waliambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Wakala hiyo pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.