*Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan*
#Tunaamini bila elimu hakuna maendeleo, makabidhiano ya shule
hii yanafanyika wakati muafaka ambapo Serikali inaendelea na utekelezaji wa
sera ya elimu msingi bila ada.
#Nakushuru Rais Museveni kwa wema uliotutendea kwa kugharamia
ujenzi wote wa shule hii kwa takriban Dola za Marekani milioni 1.6 mpaka
kukamilika kwake, fedha hizi ungeweza kuzitumia nchini kwako lakini kwa upendo
wako uliona Chato wana uhitaji zaidi.
#Kwa niaba yangu pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, napenda kuishukuru Serikali ya Uganda kwa kuimarisha ushirikiano
wetu, katu haujawahi kutambulika kwa mipaka ya kijiografia baina yetu ila
unatambulika kwa urafiki, ujirani na udugu wetu.
#Shule ya Msingi Museveni italeta manufaa ya kuongeza fursa kwa
wanafunzi wote kupata elimu kwani ujenzi umezingatia wenye mahitaji maalumu pia
itaimarisha utoaji wa elimu bora kwa kuwa na miundombinu yote muhimu.
#Naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuuenzi mchango
wa Rais Museveni kwa kuweka historia ya Hayati Rais Magufuli na Rais Yoweri
Museveni katika maktaba iliyopo shuleni hapo ili wanafunzi waelewe historia ya
Marais hawa waliodhamiria na kutimiza ujenzi wa shule hii.
#Suala la mwanafunzi wa kike aliyepata ujauzito na kuruhusiwa
kurudi shuleni lisitupe wasiwasi na kutupotezea muda kulijadili, tuko makini,
yale mashaka tunayoyafikiria tutayashughulikia na hayataleta madhara ndani ya
mfumo wetu wa elimu Tanzania.
# Kwa niaba ya Serikali, nakuhakikishia majengo na miundombinu
hii itatumika na kutunzwa vizuri ili iweze kuwanufaisha watoto wengi wa
kitanzania. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya Shule za
Msingi nchini kwa kushirikiana na wananchi na wadau.
*Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Watu wa Uganda, Mhe. Yoweri
Museveni*
# Kuniambia kujenga shule hii sio kwamba Tanzania ilikuwa haina
pesa ya kujenga shule hii lakini ni undugu na kumbukumbu.
*Yaliyosemwa na viongozi wengine*
#Ujenzi wa shule ya Msingi Museveni umekamilika mnamo Februari,
2021 ambapo shule hiyo ina vyumba vya madarasa 17, jengo la Utawala,maktaba,
jengo la elimu ya awali, ukumbi wa mikutano, matundu ya vyoo 37 na nyumba moja
ya walimu - Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, *Prof. Joyce Ndalichako*.
#Mkoa wa Geita una jumla ya Shule za Msingi 701 ambapo kati ya
hizo 652 ni za Serikali. Shule zitakazofundisha kwa lugha ya kiingereza
zitakuwa 52 ukijumlisha na moja inayozinduliwa leo - *Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Rosemary Senyamule*
#Shule ya Msingi Museveni tayari imesajiliwa tangu Aprili 8,
2021 na inatarajia kupokea wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza
Januari, 2022 - *Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule*
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*
Comments
Post a Comment