SHIRIKA LA NYUMBA (NHC) KUANZA KUWAONDOA WADAIWA SUGU WA NYUMBA ZAKE

 


Na Mwandishi Wetu, MWANZA

 

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  linatarajia kuanza kuwaondoa wapangaji wa nyumba zake ambao ni wadaiwa sugu kuanzia mapema mwezi Desemba 2021.

 

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wapangaji wa shirika hilo jijini Mwanza ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi kukagua utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi  na zile za shirika la Nyumba la Taifa pamoja na kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za ardhi.

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linadai takriban Bilioni 26 Kwa wapangaji wa nyumba zake jambo alilolieleza linachangia kuzorotesha kasi ya utendaji kazi wa shughuli za kila siku za shirika ikiwemo ukarabati 

 

‘’Tutachofanya sasa, yeyote aliyelimbikiza deni na tushampa notisi lakini bado halipi kodi basi zoezi la kumuondoa litafanyika bila hata kumtaarifu upya’’ Alisema Dkt Mabula

 

Aliongeza kuwa, oparesheni a kuwaondoa wadaiwa sugu wa nyumba za NHC itaenda sambamba na kuwaondoa wapangaji wote wasio waaminifu waliopangisha nyumba za shirika kwa gharama nafuu huku nao wakipangisha watu wengine kwa gharama kubwa ambapo alikielezea kitendo hicho kuwa ni kuiibia Serikali na halikubaliki kwa kuwa ni kosa kisheria.

 

Aliwahakikishia wapangaji wa Nyumba za NHC kuwa, Shirika hilo limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake ikiwa ni mpango wake wa miaka mitano na tayari kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni hamsini kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo

 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi mbali na kupongeza shughuli zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa aliliomba shirika hilo kuona namna ya kuzifanyia marekebisho baadhi ya nyumba zake hasa upakaji upya wa rangi baada ya Serikali kuwapanga upya wafanya biashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga maeneo ya miji ili kupendezesha Mji

 

Naye Meneja wa NHC   mkoa wa Mwanza Fadhili Anyegile alisema, kwa mwaka wa 2021/2022  shirika hilo limeweka mikakati ya kuhakikisha linapunguza malimbiko ya madeni ya wapangaji kwa asilimia mia moja, kutoa elimu kwa wapangaji juu utaratibu wa kulipa kodi kwa wakati na kuendelea na zoezi la kufanya matengenezo makubwa na madogo katika nyumba zake Ili kuzifanya kuendelea kuwa imara.

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.