SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

 


Na Mwandishi Wetu, MWANZA

 

Serikali ya awamu ya sita chini Rais Samia Suluhu Hasan imedhamiria kumaliza kero na migogoro ya ardhi nchini kwa kutatua iliyopo na kuweka mikakati ya kuzuia migogoro mipya ikiwemo utwaaji maeneo ya wananchi bila kulipa fidia

 

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mwishoni mwa jijini Mwanza wakati wa kutatua migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyopo wilaya ya Nyamagana ukiwemo mgogoro wa wananchi na Mwekezaji kampuni ya Pamba Engineering uliopo kata ya Mhandu.

 

Mgogoro mwingine ni baina ya Msimamizi wa Mirathi Ndugu Abuu mwana familia ya Marehemu Mzee Seif eneo la Miembeni mtaa wa Nera kata ya Isamilo kuhusu umilikishwaji eneo lao la urithi na ulipwaji fidia kwa wananchi wa mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele kutokana na Serikali kutwaa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa shule 

 

Katika kutatua mgogoro kati ya wananchi na Mwekezaji Pamba Engineering Naibu Waziri Dkt Mabula ameelekeza wananchi kumilikishwa eneo linalolalamikiwa kati yao na Mwekezaji katika Kata ya Mhandu kufuatia wananchi hao kukidhi matakwa yote ya kisheria na kulipa gharama za umilikishaji huku Familia ya Marehemu Mzee Seif ikielekezwa kupatiwa viwanja Saba vilivyopatikana baada ya kupimwa eneo lao la asili alilolinunua marehemu baba yao miaka ya themanini kwa aliyeteuliwa kusimamia mirathi baada ya kujiridhisha 

 

Kuhusu eneo la mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele Mhe Dkt Mabula mbali na kuwataka wananchi wa mtaa huo kushirikisha viongozi waliopo katika maeneo yao kutatua kero mbalimbali za ardhi alimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Sekiete Yahaya kuhakikisha anawalipa fidia wananchi wote 20 waliotwaliwa maeneo yao na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule mapema kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kuisha ambapo kiasi cha shilingi milioni 350 zinadaiwa na wananchi hao

 

‘’Nikuombe Mkurugenzi wananchi hawa wamekaa muda mrefu wakisubiri fidia wengine wameshindwa hata kuendeleza maeneo yao  kwa sababu hawajalipwa  fidia, naomba wananchi hawa walipwe wote kabla ya mwaka wa fedha wa sasa kuisha ‘’ Alisema Dkt Mabula

 

Kwa upande wake mkurugenzi wa jiji la Mwanza Sekiete Yahaya alisema kuwa,  maeneo yanayotwaliwa kwa ajili ya taasisi za Serikali kama shule na huduma nyengine yatalipwa fidia kwa awamu mpaka deni lote litakapokwisha.

 

 ‘’Mhe Naibu Waziri naahidi kulipa fidia kwa awamu kuanzia kipindi hiki cha kati kati ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kumaliza jumla ya milioni 150 kufikia mwishoni mwaka huu wa fedha’’ alisema Yahaya.

 

Naye Diwani wa kata ya Luchelele Vicent Lusana alifafanua kuwa wanafunzi wanaotoka eneo lake wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu na kusisitiza kuwa ipo haja kwa Serikali kuharakisha ulipwaji wa fidia ili waanze ujenzi wa shule kwa lengo la kuwafanya  wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu katika umbali mfupi na kuwaepusha na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni 

 

Akihitimisha Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Elia Kamihanda ametaka kuzingatiwa utengwaji maeneo kwa ajili ya shughuli za Umma katika zoezi la upimaji na upangaji wa mji huku akiwaasa wananchi kuhakikisha wanayalinda maeneo yote yanayotengwa kwa matumizi ya jamii ikiwemo malalo na maeneo ya wazi.

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.