Na Faustine
Kapama, Mahakama-Lushoto
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili na Watendaji wa
Mahakama nchini kushirikiana kwa karibu na kuacha kugombea fito na madaraka
wakati wa kutekeleza majukumu ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Siyani ametoa wito huo leo
tarehe 29 Novemba, 2021 wakati anafungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu
Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA).
“Usimamizi wa utekelezaji wa
majukumu yote yanayosaidia katika utoaji wa haki umo mabegani mwenu. Mkiwa
wamoja, imara na madhubuti katika kazi zenu, tutaifikia dira yetu kwa haraka
zaidi, vinginevyo safari yetu itakuwa ndefu. Nitumie fursa hii kusisitiza
ushirikiano, upendo, kuheshimiana na kusaidiana baina yenu ili kazi iendelee.
Msiende kugombea madaraka,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi,
makoti ya uongozi waliyovikwa na Watanzania wanapaswa kuyatumia vizuri ili
kuwaletea maendeleo, hivyo umoja miongoni mwa viongozi ni muhimu katika
mafanikio ya aina yoyote. Alibainisha kuwa kwa kuwa viongozi hao wanajenga
nyumba moja, hakuna sababu ya kugombea fito, hivyo ni budi kuwa kitu kimoja.
Mhe. Siyani aliwakumbusha viongozi
hao jambo jingine muhimu linalohusu uhuru wa Mahakama, huku akibainisha kuwa
uhuru unaokusudiwa sio ule wa kuifanya Mahakama ya Tanzania kuwa kisiwa. “Sisi
tumekasimiwa jukumu la kusimamia haki nchini na uhuru wetu ni kwenye kuamua juu
ya haki za watu. Uhuru huo unapaswa kulindwa kwa kusudi la kujenga na sio
kubomoa. Ni vema kila mmoja wetu akaheshimu na akaulinda uhuru huo lakini pia
kuheshimu mipaka ya mihimili mingine,” alisema.
Jaji Kiongozi alibainisha pia kuwa
Mahakama inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano wenye nguzo kuu tatu
ambazo ni Utawala, Uwajibikaji na Matumizi ya Bora ya Rasilimali; Upatikanaji
wa haki sawa kwa wote na kwa wakati; na Kujenga taswira chanya na Kurejesha
imani ya wananchi kwa Mahakama. Hivyo, aliwasihi katika utendaji wao kuzingatia
nguzo hizo zote kwa uaminifu, bidii na uadilifu, kila mmoja kwa nafasi yake na
kuonya kuwa matokeo ya kazi za kila mmoja wao yatapimwa kwa kutumia nguzo hizo
tatu.
Mhe. Siyani alisema kuwa kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama ina wajibu wa
kutoa haki kwa wote na kwa wakati kama inavyoelezwa katika Ibara ya 107A na ili
kuweza kutekeleza majukumu ya utoaji haki vema viongozi wote hawana budi kuwa na uelewa wa
kutosha juu ya masuala ya sheria na haki kwa ujumla. Alikumbushia kuwa Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa
watumishi wote wa Mahakama wanatakiwa kuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha wa
majukumu yao na nafasi zao.
“Hivyo, ni kwa muktadha huo
mafunzo haya yameandaliwa ili kuweza kutimiza hitaji la kikatiba Pamoja. Binafsi nimepata nafasi ya
kupitia ratiba yenu ya mafunzo kwa siku tano zijazo. Nimefurahi kuona kuwa mada
zilizopo katika ratiba hiyo zinalenga kutukumbusha yatupasayo kufanya ili
kutimiza nguzo hizo tatu za Mpango Mkakati,” Jaji Kiongozi alisema.
Akitoa neno la shukrani, Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alishukuru uongozi wa Mahakama
na Chuo kwa ujumla kwa kuwezesha mafunzo hayo, huku akiahidi kwa niaba ya Naibu
Wasajili na Watendaji kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Jaji Kiongozi katika
kuwatumikia Watanzania wakati wakitekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa
umma.
“Tutafanya yote tutakayoweza kwa
kadri tutakavyojaliwa kuweza kutimiza malengo ya kitaasisi. Migongano( baina ya
viongozi) inaweza kuwepo, kama ambavyo hata kwenye vitabu vya dini wanasema
majaribu hayanabudi kuja, ila ole wake ayaletaye,” alionya Mhe. Chuma.
Akitoa neno la salamu kabla ya
Jaji Kiongozi kufungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili
mkubwa, hivyo kuwa na watu sahihi, wenye taaluma sahihi na wabobezi sahihi ni
jambo la msingi sana, hivyo hawatapoteza chochote katika kuwekeza katika uelewa
wa watu. Alimhakikishia Jaji kiongozi kuwa sio kwa Naibu Wasajili tu na
Wakurugenzi Wasaidizi waliojiunga hivi karibuni, bali pia Mahakama itaendelea
kutoa mafunzo kwa kada zote.
“Nimeshaongea na Mkuu wa chuo
watengeneze program fupi ya mafunzo kwa ajili ya makatibu muhtasi, watunza
kumbukumbu na pia madereva wetu ambao wakati sisi tumelala kwenye magari wao
wanatuendesha masaa yote, angalau nao waje Lushoto ili waweze kufurahia kazi
zao wanazofanya. Nina amini hilo litafanyika,” alisema.
Katika mafunzo hayo, mada
mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali,
akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu Mstaafu ,Mohamed Chande
Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na watendaji wengine
waandamizi wa Mahakama.
Miongoni mwa mada
zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa Kimkakati, Stadi
za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa Mahakama, Utamaduni wake
na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama
na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili
ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya Umma pamoja na Usimamizi wa
Nyaraka.
Comments
Post a Comment