Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Timu za Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya
Mifugo na Uvuvi zimeibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa
wanaume na wanawake kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo kwa Idara na
Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Mchezaji Tuombe Alphonce wa Wizara ya Maji
alimshinda Stephano Mjema wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika mchezo wa
fainali kwa pointi 2-1; huku Sakina Chamshama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
amemfunga Stella Telengelwa wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa pointi 2-0.
Nafasi ya tatu kwa wanaume imechukuliwa na Abdu
Chalamande wa RAS Shinyanga aliyemshinda Paschal Banzi wa Wizara ya Katiba na
Sheria kwa alama 2-0; wakati kwa wanawake aliyeshika nafasi ya tatu ni
Ambiliasia Minja wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) aliyemfunga
Mayasa Mlula wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera.
Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba kwa
wanawake uliokuwa hatua ya Nane bora timu ya Idara ya Mahakama waliwavuta
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa 2-0; nayo Ofisi ya Waziri Mkuu Sera waliwavuta
Hazina kwa 2-0; huku RAS Iringa waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta
ya Uchukuzi) kwa 2-0 na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
waliwashinda Wizara ya Mambo ya Ndani kwa 2-0.
Mechi hizo za nusu fainali zitafanyika kesho
ambapo kwa wanaume timu zilizofuzu ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta
ya Uchukuzi), Idara ya Mahakama, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mh. Martin Shigela jana
amesema hakuna sababu kwa mwaka 2022 timu zilizoshiriki mwaka huu kushindwa
kushiriki na badala yake ziongezeke Zaidi ili kuleta ushindani mkubwa baina ya
timu, ambapo pia watumishi wanaposhiriki wanaongeza ufanisi mahala pa kazi
kutokana na kuwa na afya njema.
“Mtumishi wa Umma anapoingia kwenye mashindano
anajengewa uwezo wa kufanya kazi kwa makini na bidii, hiyyo wanapokuja kucheza
katika mashindano kunawaongezea vitu Fulani akilini na mwilini mwao,” amesema
Mh. Shigela.
Wakati huo huo, mchezo wa kuendesha baiskeli itafanyika kesho kwa upande wa
wanawake ni kilometa 24.5 zitakazoanzia Njiapanda ya Kilosa na kumalizikia eneo
la Mafiga, huku kwa wanaume ni kilometa 35 zinazoanzia Kijiji cha Malecela na
kumalizia eneo la Mafiga.
Mwisho
Comments
Post a Comment