Na Mwandishi Maalum – Dodoma
28/10/2021 Watumishi wa afya
nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO – 19 kwani wapo katika nafasi kubwa ya kupata maambukizi
ya ugonjwa huo kupita wagonjwa wanaowahudumia ukilingaisha na watu wengine.
Rai hiyo imetolewa leo jijini
Dodoma na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akitoa elimu ya chanjo kwa watumishi wa afya wa hospitali ya
taifa ya magonjwa ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma
kilichopo chini ya hospitali hiyo.
Prof. Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango
wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi
ya UVIKO – 19 alisema mwitikio wa wataalam wa
afya kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe umekuwa mkubwa na
elimu waliyoipata itawasaidia kuwa mabalozi wazuri katika jamii zinazowazunguka
na kuwafanya wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 .
“Wataalam wa afya ukiacha kwamba tupo hospitali kwa muda mwingi
pia tupo katika nafasi kubwa ya kupata ugonjwa wa UVIKO – 19 hii ni kutokana na mazingira tuliyonayo hivyo kuziweka familia
zetu katika hatari ya kupata ugonjwa huu, ni vyema tukapata taarifa sahihi na
kuwa mstari wa mbele kuchanja na kulinda afya zetu”, alisema Prof. Janabi
“Leo hii nimetoa elimu kwa wahudumu
wa afya kwasababu tuna imani kubwa wafanyakazi wa afya wakiwa na uelewa wa
kutosha na kujitokeza kuchanja itatoa motisha pia kwa jamii kujitokeza
kwa wingi lakini pia watakuwa wahamasishaji wakubwa kutoa elimu hiyo ya
kisayansi kwa wananchi wanaowazunguka”, alisema Prof. Janabi.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa
Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe Dkt. Japhet Swai alisema
wafanyakazi wa Mirembe wamekuwa na shauku ya kupata elimu kama waliyoipata
kupitia Prof. Janabi ambayo kwa hakika itafuta rekodi ya wataalam kutoka
Hospitali ya Mirembe ya kuwa nyuma katika suala ya kuchanja chanjo ya UVIKO – 19.
“Kati ya watumishi 190 tulionao
watumishi waliochanja hadi sasa ni 28 tu kutokana na maswali mengi ambayo
yalikuwa hayajapatiwa ufumbuzi lakini sasa ujio wa Prof. Janabi umekuwa ni
bahati kwa watumishi wa Mirembe kupatiwa ufumbuzi wa maswali waliyokuwa nayo,
naamini sasa watajitokeza kuchanja na kuelimisha jamii inayowazunguka”, alisema
Dkt. Swai
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya
akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe na Mkuu wa Kitengo
cha Mafunzo na Tafiti Innocent Mwombeki alisema amepata elimu mpya kuhusu
chanjo ya UVIKO –
19 ambayo sasa anaweza kuitoa na
kuipeleka kwa wafanyakazi wenzake ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote
wamejikinga na ugonjwa huo pamoja na kujitokeza kuchanja.
“Maswali mengi ambayo watu wamekuwa
nayo katika jamii kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 leo tumepata majibu yake kupitia elimu iliyotolewa na Prof.
Janabi hivyo naamini elimu hii itasaidia sana kupunguza hofu waliyokuwa nayo
wafanyakazi wa afya na kuwapa motisha ya kujitokeza kuchanja”, alisema Dkt.
Mwombeki.
Naye mwanafunzi wa udaktari bingwa
wa magojwa ya akili wa mwaka wa pili katika Hospitali ya Mirembe Suluma
Aslan alisema chanjo ya UVIKO – 19 ilivyoingia
nchini aliogopa kuchanja kutokana na hali yake ya ujauzito aliyokuwa nayo
kwamba ungemletea shida yeye pamoja na mtoto wake lakini baada ya elimu sahihi
ya chanjo amekuwa ni miongoni mwa watu waliochanja siku ya leo.
Takwimu zinaoesha kuwa hadi sasa
chanjo karibu bilioni 6.9 zimeshatolewa na nusu ya dunia imeshachanja wakati
Bara la Afrika asilimia 3 ya watu ndio waliopata chanjo.
Mwisho
Comments
Post a Comment