Na Munir
Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Wataalam wa
Mipangomiji nchini kuhakikisha wanapopanga mipango yao kwenye maeneo mbalimbali
nchini wanatenga maeneo ya wafanyabiashara wa kawaida ili waweze kufanya
biashara katika mazingira rafiki na yaliyo bora.
Alisema, baada ya
Wataalam hao kutekeleza wajibu wao wa kupanga, halmashauri nchini ambazo ni
mamlaka za upangaji ziweke miundombinu ili wafanyanyabiashara hao wapatikane
kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa kawaida ni sharti
yawe na huduma zote muhimu kama vile maji, umeme na barabara ili kuwawezesha
kufanya biashara zao hata usiku kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
‘’Mnapoandaa michoro
yenu ya mipangomiji zingatieni taaluma huku mkikumbuka kuna makundi maalum kama
vile Mamalishe, Machinga, Bodaboda na watanzania wa kawaida na muwawekee
utaratibu maalum wa kupata ardhi kwa gharama nafuu ili nao waweze kushiriki
kujenga maeneo yaliyopangwa’’ alisema Naibu Waziri Dkt Mabula
Akizungumza wakati wa
kufunga Mkutano Mkuu wa Saba wa Wataalamu wa Mipangomiji uliofanyika tarehe 27
Oktoba 2021 mkoani Morogoro, Naibu Waziri Mabula alisema, mipango ya
uendelezaji miji na michoro ya mipangomiji inapoandaliwa ipelekwe mitaani
katika lugha ambayo wana mitaa wanaweza kuielewa.
‘’Mipango ya uendelezaji
miji inapoandaliwa iletwe mitaani katika lugha ambayo wana mitaa wanaweza
kuielewa ili waweze kusimamia, sababu wao ndiyo wadau na watasaidia hata katika
development control’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, aliwataka
Wataalam wa Mipangomiji kushirikisha watendaji kata, mitaa na vijiji katika
mipango ya uendelezaji mji kwa kuwa wao ndiyo wadau muhimu na kusisitiza kuwa
wadau hao ni nguvu kazi itakayosaidia kupunguza ujenzi holela kwenye maeneo ya
mijini na vijijini.
Naibu Waziri wa Ardhi
aliwaasa Wataalam Mipangomiji kuwa wabunifu na kuandaa miradi shirikishi
isiyokuwa na suala la fidia na kubainisha kuwa miradi hiyo ni lazima
itafanikiwa kwa kuwa itakuwa imeshirikisha wananchi watakaojiona kama sehemu ya
wamiliki wa miradi hiyo.
Pia aliitaka Bodi ya
Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji kuendelea kusimamia nidhamu, maadili na
uwajibikaji kwa wataalamu wa sekta hiyo ili kuleta ufanisi katika sekta ya
mipangomiji.
Awali Mwenyekiti wa Bodi
ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji Profesa Wilbard Kombe alimueleza Naibu
Waziri wa Ardhi kuwa, katika maazimio yake wajumbe wa mkutano huo walipendekeza
kufanyika mabadiliko kwenye sheria namba nne kwenye kifungu kinachohusu mfuko
wa fidia ili watumiaji wakubwa wa ardhi wachangie mfuko huo.
‘’Tumeona huu ni wakati
muafaka kwa watumiaji wakubwa wakachangia katika huu mfuko ili kuipa nguvu
wizara kumudu gharama zinazotokana na fidia hasa baada ya ardhi kuwa na
thamani, kutegemea wizara moja kumudu jukumu hili ni ngumu sana hivyo tumeona
ni wakati muafaka kufanya mabadiliko kwenye sheria hiyo’’ alisema Kombe.
Mkutano huo wa Wataalam
wa Mipangomiji nchini wenye kauli mbiu ‘Mipangomiji na Uwekezaji Shirikishi
Tanzania’ ulishirikisha Wataalamu wa Mipangomiji 230 kutoka mikoa mbalimbali
nchini na ulifunguliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi.
Comments
Post a Comment