Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ametembelea kambi ya Timu ya
Wizara ya Ardhi iliyoko Mazimbu mkoani Morogoro kwa lengo la kuwapa hamasa
wachezaji wa timu hiyo wanaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi katika mashindano hayo inawakilishwa na timu mbili za mpira
wa miguu na mpira wa pete (Netball) na timu hizo zimeanza kufanya vizuri katika
michezo yake ya awali.
Katika michezo yake ya awali timu ya mpira wa miguu
ya Wizara ya Ardhi Ilizifunga timu za Katiba 1-0 na TARURA magoli 3-0 wakati
timu ya mpira wa pete ikiifunga Uchukuzi kwa point 14-13 na Kilimo 23-12 na
kutoka sare ya 23-23 na NFRA.
Akizungumza na wachezaji wa timu hizo tarehe 28
Oktoba 2021 mkoani Morogoro, Naibu Waziri Dkt. Mabula
aliwataka wachezaji wa timu hizo kujituma na kuwa na nidhamu katika kipindi
chote cha mashindano ili waweze kupata ushindi na hatimaye kurudi na vikombe.
“Cha kuzingatia wakati wa kushiriki mashindano haya
ya SHIMIWI ni kuwa na nidhamu pamoja na kujituma ili muweze kuibuka washindi
katika mechi zenu na hatimaye mrudi na vikombe’’ alisema Naibu Waziri Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula,
mbali na michuano ya SHIMIWI kushindanisha Wizara na Idara za Serikali kwa
lengo la kupata washindi lakini michuano hiyo inasaidia kuimarisha afya za
watumishi na wakati huo kujenga mahusiano baina ya watumishi.
MWISHO
Comments
Post a Comment