Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya
kujiepusha kutumia usafiri wa wananchi wanaoshitakiana wakati wa kwenda
uwandani ili kuepuka tuhuma za kufanya upendeleo wakati wa kusikiliza mashauri.
Dkt. Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 27 Oktoba, 2021
mkoani Morogoro wakati akishuhudia uapishwaji wajumbe wapya wa Baraza la Ardhi
na Nyumba la Wilaya ya Morogoro uliofanywa na Mkuu wa mkoa huo Martine
Shigela. Baraza la Ardhi na Nyumba la Morogoro linahudumia halmashauri
tatu za Mvomero, Morogoro Vijijini na Manispaa ya Morogoro.
"Ninaomba hili mliepuke sana maana linaleta
changamoto kubwa, na mwingine anaweza akakata rufaa akidai mwenzake alikuwa
anawapeleka wajumbe uwandani, suala hilo limekuwa likileta shida sana’’ alisema
Dkt. Mabula.
Wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya wana
jukumu la kusikiliza kesi na kutoa maoni juu ya shauri husika kwa maandishi na
wakati wa kusikiliza shauri wana wajibu wa kuhoji maswali ya ufafanuzi ili
kupata uelewa zaidi.
Maoni ya wajumbe yanatumika kumsaidia Mwenyekiti wa
Baraza kutoa maamuzi ingawa ni lazima Mwenyekiti ajikite katika sheria hivyo
anaweza kuyakubali maoni hayo au kuyakataa lakini lazima atoe sababu za
kuyakataa.
Dkt. Mabula alisema, Wizara inachoshauri ni
Mwenyekiti wa Baraza awe na ratiba ya mwezi mzima kuhusiana na safari za kwenda
uwandani na taarifa iwasilishwe kwa Mkuu wa wilaya pamoja na Mkurugenzi
wa Halmashauri husika ili inapofika siku ya kwenda uwandani basi watumie
usafiri wa serikali.
Aliongeza kwa kusema kuwa, kutumia usafiri wa
serikali kutaepusha minong’ono na kumkosesha amani mmoja wa miongoni mwa
wanaoshitakiana kwa kuhisi kuwa anaweza kuwa anaonewa.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ametaka mashauri katika Mabaraza ya Ardhi kumalizika katika kipindi
kisichozidi miezi sita labda kwa yale mashauri ambayo yanaweza kucheleweshwa
kwa sababu za mawakili.
"Naomba katika kupangilia kesi zisiwe zinapelekwa
mbali sana kiasi cha kujikuta mtu anasota mwaka mmoja, miaka miwili kesi
haijaisha tutakuwa hatiujawatendea haki’’ alisema Dkt. Mabula.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela
aliwapongeza wajumbe wa Baraza walioteuliwa na kuwaeleza kuwa uteuzi walioupata
umezingatia uadilifu na weledi wao na ana matumaini wajumbe hao wataenda
kutenda haki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
‘’Nina matumaini katika nafasi hii mliyoipata
mtaenda kutenda haki katika mashauri kwa watu watakaofika kwenye Baraza la
Ardhi na Nyumba na hatutarajii kuona uadilifu unapungua mahali ambapo wananchi
wanaenda kupata haki kuwa sehemu ya kuilalamikia’’ alisema Shigela.
Jumla ya wajumbe wanne wa Baraza la Ardhi na Nyumba
la wilaya ya Morogoro waliapishwa kuhudumu kwenye baraza hilo na sababu ya
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kuketi na wajumbe katika kusikiliza mashauri ni
kushirikisha jamii kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi na wajumbe hao wana
msaada mkubwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na
Nyumba la Wilaya ya Morogoro Mwanahawa Kassim hadi kufikia septemba 2021 katika
wilaya ya morogoro Manispaa, Morogoro Vijijini na Mvomero kuna jumla ya
mashauri 1,220 ambapo kati ya mashauri hayo yaliyofunguliwa kwa mwezi
septemba pekee ni 57 na yaliyoisha mwezi huo ni mashauri 114.
Comments
Post a Comment