UJENZI WA UWANJA WA NDEGE MSALATO WAANZA DODOMA

Na Rhoda Simba, Dodoma

 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha kuwa wanasimamia ujenzi wa kiwanja cha Ndege cha kimataifa cha Msalato ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.



 

Waziri Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo jijini hapa mara baada ya kutiliana saini na Mkandarasi mkataba wa mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).

 

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutawezesha kutua kwa Ndege kubwa kama vile Airbus pamoja na Dreamliner katika Mkoa wa Dodoma. “Pia kiwanja hiki kitafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Mkoa wa Dodoma hivyo, TANROADS muhakikishe kuwa mkandarasi mnamsimamia ipasavyo ili kumaliza kazi hii kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa” ameagiza Prof. Mbarawa.

 

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila, akitoa taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho, amesema kitajengwa kwa awamu mbili.

 

“Awamu ya kwanza inahusisha kazi kuu mbili ambazo ni ujenzi wa barabara ya kuruka ndege na ujenzi wa majengo ikiwemo jengo la abiria” amesema Mtivila.

 

“Mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua Ndege ni Sinohydro Corporation Limited in JV with M/S Beijing Sino-Aero Construction Engineering Co., Ltd and M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation CO. Ltd kutoka China” amesema Mtivila.

 

Pia, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itakapo kamilika kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka. “Mheshimiwa Waziri awamu ya pili ya mradi itatekelezwa kwa kutegemea mahitaji yatakayojitokeza ndani ya kipindi cha miaka 20, baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kukamilika” amesema Mtivila.

 

Aidha, amesema mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho cha kimataifa Msalato, unatekelezwa kwa ufadhiri wa benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kwa fedha za mkopo nafuu.

 

Amesema AFDB, watatoa jumla ya Dola milioni 329.47 na serikali ya Tanzania itagharamia Sh. bilioni 127 ambapo fedha zitakazo changiwa na serikali ni pamoja na malipo ya fidia kwa wananchi watakao pisha ujenzi wa mradi.

 

Kadhalika amesema ujenzi wa kiwanja hicho utakapokamilika utarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka na kuingia katika jiji la Dodoma na kati ya Tanzania na nchi mbalimbali, kukuza utalii, uchumi na kuongeza ajira.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, amesema kitendo cha wizara hiyo kutiana saini mkataba wa ujenzi kimejibu maswali mengi yalikuwa yakihojiwa na wananchi juu ya hatima ya uwanaja huo. “Watu baada ya hayati Rais Magufuli kufariki waliona kama miradi hii ambayo alikua ameiasisi haitatekelezwa tena lakini leo hii tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan, ameweza kujibu maswali ya watu wengi” alisema Kakoso.

 

Vilevile, amesema kamati hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.

 

MWISHO

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.