TEA KUSIMAMIA UANZISHWAJI WA MIFUKO YA ELIMU KWENYE HALMASHAURI ZOTE NCHINI

Na Eliafile Solla, TEA


Miundombinu bora ya elimu katika Halmashauri nyingi hapa nchini ni changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo.

 


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati. I. Geuzye akiwasilisha nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma


Kauli hii imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati. I. Geuzye, alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Awali ya yote Bi. Bahati alibainisha kwamba, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatambua umuhimu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika kuhamasisha na kuboresha mahusiano yao ya kiutendaji na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji kote nchini.

‘‘Kutokana na changamoto hizo za miundombinu bora ya elimu, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo inaratibu na kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeandaa utaratibu utakaowezesha Halmashauri zetu kuanzisha Mifuko ya Elimu na kwa zile Halmashauri ambazo tayari zina mifuko hiyo tuna dhamira ya kuihuisha na kuanza kuitumia kikamilifu’’, alisema Bi. Bahati.

Aliongeza kwamba, katika mwaka 2020 sheria ndogo ya uanzishwaji wa Bodi ya Mfuko wa Elimu wa Halmashauri iliridhiwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na vile vile mwongozo wa uanzishwaji wa Mifuko umekwishaandaliwa na kusambazwa kwa wajumbe hao wa mkutano wa ALAT.

‘‘Kazi iliyopo mbele yetu ni kutekeleza lengo kuu la kuanzisha na kuhuisha Mifuko ya Elimu katika Hamlashauri zote nchini, moja ya mipango inayolenga uboreshaji wa elimu katika maeneo wanayoishi wananchi’’ alibainisha Bi. Bahati

Zoezi hili la uanzishwaji na uhuishwaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri lina faida nyingi ikiwemo kuwezesha Halmashauri kukuza ushirikiano wa jamii katika kuchangia miradi ya kipaumbele ya elimu; kuboresha, kuendeleza na kukuza viwango vya elimu katika Halmashauri husika.

Vile vile mifuko hii itawezesha Halmashauri kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya miradi ya elimu ndani ya Halmashauri pamoja na kuratibu upatikanaji wa michango kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kiserikali, mashirika ya kidini na watu binafsi kwa ajili ya kusaidia uendelezaji wa miradi ya elimu ndani ya Halmashauri hiyo.

 

 



 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.