Na. WAMJW - Dodoma
Katika kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani
kila mwaka ifikapo tarehe 28 ya kila mwezi Septemba, Wizara ya Afya
imewatahadharisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unaweza
kusababisha vifo.
![]() |
Dkt. James Kiologwe |
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa
Yasiyo ambukiza, Dkt. James Kiologwe akitoa Tamko la Serikali kwa niaba ya
Katibu Mkuu katika kuadhimisha siku ya ugonjwa huo Duniani.
“Kwa mwaka huu kati ya mwezi Januari hadi Agosti,
watu 39,787 wametolewa taarifa ya kung’atwa na mbwa au wanyama wa jamii hiyo
ikiwa ni ongezeko la zaidi ya watu 5,000 ukilinganisha na kipindi kama hicho
cha mwaka uliopita” amesema Dkt. James Kiologwe na kuendelea kusema kuwa
takwimu hizo hazijumuishi matukio yaliyotokea katika vituo vya kutolea huduma
bila kutolewa taarifa au yaliyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika
katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo tatizo hilo ni linaweza kuwa
kubwa kuliko tunavyofikiri” amefafanua zaidi Dkt. James Kiologwe.
Ameitaja Mikoa inayoongoza kuwa ina idadi kubwa ya
wagonjwa kuwa ni Mkoa wa Morogoro ambao una wagonja 4329 ukifuatiwa na Mkoa wa
Dodoma wenye wagonjwa 4233.
“Waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya
miaka 15 na hii inaweza kuwa ni kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa
(anayefugwa) muda mwingi, na pia hupenda kucheza au kuchokoza mbwa
wasiowafahamu njiani” amesema Dkt. Kiologwe.
Dkt. James amesema kuwa Ugonjwa wa kichaa cha mbwa
husababishwa na Kirusi wa Kichaa cha Mbwa (Rabies Virus) kutoka kwa wanyama
jamii ya mbwa ambao wameathirika na kirusi hiki (Mbwa, paka, mbweha, fisi na
wengineo) na humwingia mwanadamu kupitia mate ya mnyama huyo kuingia katika
jeraha na dalili huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa
fahamu, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa,
maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa mate mengi mfululizo,
kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimae kupoteza
maisha. Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi na imani potofu za
kishirikina.
“Endapo mtu ameng’atwa na mbwa, hatua ya kwanza
muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririkika
na sabuni. Kidonda kisifungwe na kisha apelekwe au afike haraka katika kituo
cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa” amesema
Dkt. James Kiologwe.
Amesisitiza kuwa ni muhimu aliyeng’atwa na mbwa
afanyiwe tathmini ya kina katika kituo cha kutolea huduma ili aweze kupatiwa
chanjo kamili na iwapo chanjo itatolewa ni budi kumaliza kozi zote za
chanjo.
Ameendela kusema kuwa wanyama jamii ya mbwa, paka
wasiruhusiwe kulamba vidonda, kwani mate yao huweza kuleta maambukizi endapo
wameathirika, huku Wamiliki wa mbwa wahakikishe wanachanja mbwa wao dhidi ya
ugonjwa wa kichaa cha mbwa mara moja kila mwaka na kupata cheti.
Amesema kuwa mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana
na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana
na mnyama aliyeambukizwa pamooja na kuhakikisha mazingira yote ni safi,
ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunayoishi.
Ametoa rai kwa wazizi kutoa elimu kwa watoto na
kuwakataza kuchokoza mbwa wasiowajua (mfano: kuvuta mkia au masikio,
kumpanda mgongoni)
Amesema kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikia na sekta
nyingine ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM) - Dawati
la Afya Moja pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Chakula
Duniani (FAO) pamoja na wadau mbalimbali wamefanya juhudi mbalimbali za
kudhibiti ugonjwa huo na kuhakikisha inapunguza ukubwa wa tatizo linalohusiana
na ugonjwa huo kwa; Kutoa elimu kwa umma; Kuboresha dhana ya Afya Moja nchini;
Kurahisisha upatikanaji wa huduma ya chanjo ya Kichaa cha Mbwa kwa wananchi;
Kurahisisha upatikanaji wa huduma ya chanjo kwa kwa wanyama hasa mbwa.
“Serikali inatambua gharama kubwa za upatikanaji wa
chanjo, hata hivyo kupitia WAMJW, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali
za Mitaa (OR-TAMISEMI) na sekta nyingine imeweza kuchangia gharama za
upatikanaji wa chanjo ili ziwafikie wananachi kwa gharama wanazoweza kumudu”
amesema Dkt. James Kiologwe.
Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau
katika kutekeleza mikakati na juhudi za pamoja za sekta zote zinazohusika
kudhibiti ugonjwa huo inaandaa ‘Mkakati wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa’
wenye lengo la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.
MWISHO.
Comments
Post a Comment