NAIBU WAZIRI AWATAKA WATUMISHI WA ARDHI KUONGEZA KASI YA UTOWAJI HATI

Na. Hassan Mabuye, Dodoma

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula amewataka watumishi wa sekta ya ardhi wa mkoa wa Dodoma kuongeza kasi ya uandaaji na utowaji hatimiliki za ardhi kwa wananchi.

Dkt. Mabula ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki hii wakati alipokutana na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya ya Kondoa, Chemba, Bahi na Chamwino katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya sekta ya ardhi katika wilaya hizo za mkoa wa Dodoma.

Ameelekeza, kila ofisi ya halmashauri katika mkoa wa Dodoma kuandaa na kutoa angalau hatimiliki za ardhi 100 kila mwezi kwa kuwa kuna baadhi ya halmashauri ambazo amezitembelea na amekuta zinatoa zaidi ya hatimiliki za ardhi 300 katika kila mwezi.

“Huwezi kuwa na lengo la kuandaa hati 120 kwa mwaka, haiwezekani hata kama kungekuwa na mtumishi mmoja, haiwezekani. Nendeni mkapitie upya malengo yenu, labda mgeniambia haya ni malengo ya miezi mitatu sawa lakini sio malengo ya mwaka mzima”

Naibu Waziri Mabula alitoa muda wa hadi kufikia tarehe 21 Oktoba 2021 halmashauri hizo zijipange kuanza kuoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za umiliki wa ardhi kwa hati na amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma kufuatilia kwa karibu.

Aidha, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Thadei Kabonge amewataka watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Dodoma kuepuka kuzalisha migogoro mipya hasa ile migogoro ambayo inazalishwa na uzembe wa watumishi wenyewe kwa kuwa inachangia katika kuchelewesha umilikishaji wa ardhi kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma, Swaumu Muganyizi amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuwa waadilifu na kuboresha utowaji huduma kwa wananchi na kuepuka rushwa hasa katika umilikishaji.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.