Na. Omary Mtamike, MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Juma Homera amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote zilizopo mkoani
kwake kutenga bajeti ya maziwa kwa wanafunzi wote wa shule za awali na msingi
waliopo mkoani humo.
Homera ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Siku ya unywaji maziwa shuleni
ulimwenguni ambayo kitaifa imefanyika leo (29.09.2021) mkoani Mbeya amesema
kuwa suala la unywaji maziwa shuleni kwa wanafunzi ni la lazima na si hiyari.
“Hatuwezi kusubiri
wadau tu kila siku wajitoa wakati watoto ni wetu wenyewe hivyo ni lazima wakati
wa kupanga bajeti zote za halmashauri zilizopo mkoani Mbeya iwekwe bajeti ya
kutekeleza mpango huu na kwa sababu mimi ndo naidhinisha bajeti
zote,sitopitisha bajeti yoyote ambayo haina bajeti ya kutekeleza mpango huo” amesema Homera.
Aidha, Homera amepongeza juhudi na kazi inayofanywa na Wizara ya
mifugo na Uvuvi kupitia bodi ya maziwa kwa kuwa karibu na wadau mbalimbali wa
tasnia ya maziwa waliopo mkoani humo ambapo amewataka wasindikaji wote wa
maziwa nchini kuendelea kuwekeza katika mkoa huo.
“Mimi ninapenda sana
wawekezaji na kipekee kabisa niwashukuru ASAS kwa kuamua kuja kujenga kiwanda
kikubwa cha maziwa hapa, niwaombe Tanga Fresh na makampuni mengine ya maziwa
kufanya hivyo pia ili kuchochea zaidi uwekezaji katika tasnia ya maziwa katika
mkoa wa Mbeya” amesisitiza Homera.
Akizungumzia hali ya
uwekezaji kwenye tasnia ya maziwa nchini, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Stephen Michael amesema kuwa hadi sasa Tanzania ina
jumla ya ng’ombe wa maziwa Mil. 1.2 ambao huzalisha jumla ya lita za maziwa
Bil.3.1. “Aidha hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu, Tanzania ilikuwa na jumla ya
viwanda vya kusindika maziwa vikubwa, vidogo na vya kati 104 na kati ya hivyo
96 ndo vinafanya kazi” Amesema Michael.
Akibainisha kuhusu
uwezo wa uzalishaji wa viwanda hivyo, Michael amesema kuwa viwanda vilivyopo
vina uwezo uliosimikwa wa kusindika lita 865600 kwa siku lakini kutokana na
uhaba wa upatikanaji wa malighafi viwanda hivyo vinasindika wastani wa asilimia
24 ya uwezo wake ambao ni sawa na lita 206849 kwa siku.
Akielezea kuhusu
utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni, Msajili wa Bodi ya Maziwa
nchini (TDB), Dkt. George Msalya
amesema kuwa mpango huo ulianzia mkoani Kilimanjaro mwaka 2007 kwa lengo la
kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwa kujenga utamaduni huo kuanzia ngazi ya
shule ya awali.
“Tunafanya hivi kwa
sababu mbali na maziwa kuwa lishe nzuri na kiburudisho kwa watoto, imethibitika
kuwa maziwa ni mlo kamili unaoweza kujitosheleza bila kutegemea chakula kingine
na ndo chakula pekee chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini” Amesema
Dkt. Msalya.
Aidha, Dkt. Msalya amebainisha kuwa tangu kuanza kwa mpango huo
takribani watoto elfu 90 kutoka shule 210 hapa nchini wamepatiwa maziwa ambapo
amesema kuwa idadi hiyo imeendelea kupungua kadri miaka inavyoendelea. “Tunaendelea
kufanya jitihada kubwa katika kuwajengea uwezo wanafunzi, wazazi na walezi wao
juu ya umuhimu wa maziwa ili kuhakikisha kiwango cha matumizi ya bidhaa hiyo
kinaongezeka” amehitimisha Dkt. Msalya.
Maadhimisho ya Siku
ya unywaji Maziwa mwaka huu yalitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii
ikiwa ni pamoja na ugawaji maziwa katika vituo vya afya, mahabusu ya watoto na
kwenye vituo vya watoto yatima.
MWISHO
Comments
Post a Comment