Na. Revocatus Kassimba, SUMBAWANGA
Wazee wa Mkoa wa Rukwa wameiomba serikali
kuwasaidia kupata nafasi ya kusikilizwa ili wawe na uwezo wa kuchangia jitihada
za maendeleo pamoja na kuhakikisha wanapata huduma muhimu za kijamii.
Mwenyekiti mpya wa Baraza la Wazee Mkoa wa Rukwa Benedict Makosi (kushoto) akiwa na Makamu Mwenyekiti Desderius Sikazwe (katikati) na Katibu wao Amabilis Mpepo jana mara baada ya kumalizika uchaguzi |
Hayo yamebainishwa kwenye uzinduzi wa baraza la
Wazee wa Mkoa wa Rukwa jana mjini Sumbawanga ambapo pia walifanikiwa kuunda
uongozi unaoshirikisha wazee toka halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti
mpya wa Baraza la Wazee Mkoa wa Rukwa, Mzee Benedict Makosi alisema kazi ya
uwakilishi inahitaji moyo wa kujitolea na kusikiliza mahitaji ya wanachama.
“Baraza letu
lililokosa muunganiko wa wilaya zingine ikiwemo Nkasi na Kalambo kwani awali
lilihusisha wazee wa Manispaa ya Sumbawanga pekee” alisema Mzee Makosi.
Mwenyekiti huyo alitoa rai kwa viongozi wa serikali
kote mkoani Rukwa kuwa wastahimilivu na wenye moyo wa kusikiliza shida na kero
za wazee muda wote watakapopata nafasi ili maisha ya wazee na wahitaji wengine
yawe bora kama serikali inavyoelekeza.
“Uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea
hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufika uzee.
Hapa Tanzania mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo
na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika ukoo” alisema Mzee
Makosi.
Akizindua Baraza hilo la Wazee, Mkuu wa Wilaya ya
Sumbawanga Sebastian Waryuba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph
Mkirikiti alisema kuwepo kwa Taifa la
Tanzania ni kielelezo tosha cha mchango wa wazee walioutoa katika nyanja ya
kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.
Waryuba aliongeza kusema pamoja na mchango walioutoa wazee bado ni moja ya kundi lililokuwa limetengwa katika jamii na hivyo nguvu za ziada kutoka Serikalini na wadau kwa ujumla zimeendelea kufanyika ili kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi.
“Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Rukwa kwa mwaka 2021 unakadiriwa kuwa na wazee 73,361 kati yao Wanawake ni 37,509 na Wanaume ni 35,852. Aidha, kufikia Septemba 2021 Mkoa umetambua jumla ya wazee 29,905 kati yao Wanawake ni 15,954 na wanaume ni 13,951” alisema Waryuba.
Kuhusu huduma za wazee Mkuu huyo wa Wilaya alisema hadi
kufikia Septemba 2021, Mkoa umetoa jumla ya vitambulisho vya matibabu bure kwa
Wazee 16,311 sawa na asilimia 55 ya wazee wote waliotambuliwa, kati ya hao wanawake
ni 8,515 na wanaume 7,796.
Akitoa taarifa ya uchaguzi wa viongozi wapya wa
Baraza la Wazee Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala Mkoa Denis Bandisa aliwataja
waliochaguliwa na nafasi zao kwenye mabano na halmashauri wanazotoka kuwa ni Benedict
Makosi (Mwenyekiti, Manispaa ya Sumbawanga), Desderius Sikazwe (Makamu
Mwenyekiti, Kalambo) na Amabilis Mpepo (Katibu, Manispaa).
Bandisa alitaja viongozi wengine kuwa ni Melkio
Mwanakatwe (Katibu Msaidizi, Sumbawanga vijijini), Tobias Magazini (Mtunza
Hazina, Nkasi), Jenerith Umela (Mwakilishi Baraza la Madiwani, Nkasi) na
Nicolaus Lufungilo (Mwakilishi Baraza la Madiwani, Sumbawanga Vijijini).
Uundwaji wa Baraza la Wazee Mkoa ni
sehemu ya utekelezaji wa baadhi ya matamko ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na
Azimio la Umoja wa Mataifa Na.46 la 1991 kuhusu haki za Wazee ambazo ni kuwa na
uhuru, kushiriki na kushirikishwa, kutunzwa, kukuza utu wao na kuheshimiwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment