WANUFAIKA WA MRADI WA VIUNGO ZANZIBAR WAPATIWA MAFUNZO YA USINDIKAJI WA MBOGA MBOGA

 


Wanufaika wa mradi wa VIUNGO visiwani Zanzibar wameanza kupatiwa mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga na uongezaji wa thamani kwa bidhaa wanazozalisha,ikiwa ni awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ya usindikaji kupitia mradi huo.

Utolewaji wa mafunzo hayo umekuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanufaika wa mradi kujijenga zaidi kiuchumi ikiwemo kuanzisha biashara kutokana na mazao wanayozalisha.

Akitoa mafunzo hayo Afisa kilimo kupitia mradi wa Viungo Salma Nassor Marshed alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakulima kusindika mazao yao ili kukabiliana na uhaba wa masoko na kwamba sasa wataweza kuhifadhi mazao hayo bila kuharibika.

Alisema usindikaji huo pia utaongeza lishe kwa akina mama na watoto kwani wataweza kutumia mboga mboga zilizosindikwa  hata wakati wa kiangazi.

Sambamba na hayo alisema usindikaji huo pia utaongeza thamani ya fedha kwani mkulima ataweza hifadhi bidhaa alizosindika hata wakati wa kiangazi ambao matunda na mboga nyingi huadimika.

Kwa upande wake Afisa lishe kupitia mradi huo Witness William alisema mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga  yatawafikia walengwa zaidi ya elfu tano kutoka wilaya kumi  za mradi VIUNGO Unguja na Pemba.

Alisema wanufaika wa mafunzo hayo watakua na jukumu la kuwafundisha wengine ili walio wengi zaidi waweze kunufaika na elimu hio kwa maslahi ya wote.

Akifafanua kuhusu umuhimu wa usindikaji alisema wanufaika wataweza kuimarisha afya za familia zao, sambamba na kukuza kipato chao kwa kuingiza fedha zitakazotokana na mauzo ya bidhaa zao.

Kwa upande wao baadhi ya wanaufaika wa mafunzo hayo walisema yamekuja wakati sahihi ambao wakulima wengi walikosa njia sahihi za kuhifadhi mazao yao.

Walisema kwa muda mrefu wamekua wakishindwa kufahamu njia bora za usindikaji wa mazao na kufanya kilimo chao kuwa cha muda maalumu na pindi wakati wa kiangazi unapofika hawakua na hata hakiba ndogo ya mboga mgoga na matunda.


Mradi huu wa Viungo visiwani hapa unatekelezwa na PDF kwa mashirikiano ya TAMWA-ZNZ pamoja na CFP chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa muda wa miaka minne.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.