Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema
atahakikisha kila maelekezo anayoyatoa anayafuatilia kwa karibu ili
kujiridhisha na utekelezaji wake na kufikiwa kwa malengo ya serikali.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo wakati
alipofanya ziara ya kushtukiza kujionea maendeleo ya ukarabati wa machinjio ya
Jiji la Dodoma yaliyoanza Tarehe 15 Mwezi Julai mwaka huu.
Mhe. Ulega amesema ameridhishwa na ukarabati unaondelea kufanywa
ambapo hadi sasa zimetumika Shilingi Milioni 40 kwa kutumia mapato ya ndani ya
machinjio hayo.
“Kila maelekezo tunayoyatoa, tunayatoa kwa wakati maalum
na kinachofuata ni ufuatiliaji wa karibu, tunatoa maelekezo na kufuatilia
utekelezaji wake, tunawapongeza watendaji wetu wizarani maana kila maelekezo
tunayoyatoa wanayasimamia na mnafanya kazi nzuri maelekezo tunayoyatoa
mnayafanyia kazi.” Amesema
Mhe. Ulega
Mhe. Ulega amesema alitoa maelekezo ya kuona machinjio ya jiji
la Dodoma, yanabadilika na kuwa bora na kwamba ameridhika na ukarabati unaoendelea
hadi sasa ambapo awali uongozi wa machinjio ulihitaji Shilingi Bilioni Tatu,
lakini aliwaelekeza kuanza kufanya ukarabati kwa kutumia mapato ya ndani.
Amefafanua kuwa yeye kama kiongozi anatoa maelekezo na
kuhakikisha yanasimamiwa usiku na mchana na kuyafuatilia hadi mwisho wake na
kutaka maboresho hayo yawe yamekamilika kufikia Tarehe 15 Mwezi Septemba mwaka
huu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na
Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael amesema hadi sasa ukarabati
wa machinjio ya Jiji la Dodoma yamefikia zaidi ya asilimia 90 ambapo maeneo 13
kati ya 15 yatakuwa yamekamilika mwisho wa mwezi huu na maeneo mawili
yaliyobakia yatakamilika ifikapo Tarehe 15 Mwezi Septemba.
Bw. Michael amesema ni muhimu kwa wao kama watendaji
wanaposimamia maelekezo ya viongozi ni kwamba wanajua athari zinazoweza
kujitokeza kutokana na ulaji wa nyama isiyo na usalama na kwamba watasimamia
ukarabati huo kwa weledi mkubwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment