Na. Omary Mtamike, DODOMA
Aliyekuwa Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa wito kwa watendaji na
watumishi wa Sekta hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na kutenda haki wakati
wote wanapotoa huduma kwa wananchi.
Prof. Ole Gabriel
ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini kwa hivi sasa ameyasema hayo leo
(30.08.2021) katika halfa fupi ya kumuaga iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi
za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma. “Ni
vizuri muendelee kutambua kuwa nyie ni watumishi wa umma na kazi yenu kubwa ni
kutatua changamoto za watanzania kupitia sekta ya Mifugo hivyo mfanye hivyo kwa
kutenda haki bila gharama bila rushwa”.
Aidha Prof. Ole
Gabriel amemshukuru Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho kikwete na
aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli kwa kuwa wa kwanza kutambua uwezo wake na kumteua kutumikia
kwenye nafasi ya katibu Mkuu katika Wizara mbalimbali. “Ninatambua kazi
niliyonayo hivi sasa ni kubwa sana lakini ninamuahidi Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan kuwa nitaitumikia nafasi aliyoniamini kwa mafanikio makubwa na kuleta
mabadiliko anayoyatarajia katika eneo hili la Mahakama” Amesema Prof. Ole
Gabriel.
Prof. Ole Gabriel alihitimisha hotuba yake kwa kutoa rai kwa watumishi hao wote kujali afya zao wakati wote ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Uviko 19. Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wote nchini, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji (CCWT), Jeremiah amesema kuwa Prof. Ole Gabriel amefanikiwa kuwapa muongozo wa namna bora ya kukiendesha chama chao ili kiweze kuwapa manufaa wafugaji tofauti na hapo awali ambapo chama hicho kilikuwa kikijiendesha kama chama cha wanaharakati.
“Ni kwa jitihada
zako hizi ndio maana leo tumefanikiwa kutatua changamoto nyingi zilizokuwa
zikiwakabili wafugaji na kwa heshima kubwa ninaomba nikukabidhi ng’ombe mmoja
kama zawadi kutoka kwenye chama chetu” Amesema Jeremiah.
Akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya watumishi wote wa Sekta ya Mifugo, Mkurugenzi wa Idara ya
Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga
amemshukuru Prof. Ole Gabriel kwa kutenda haki na kujali usawa kwa watumishi
wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao. “Kwa kweli umekuwa ukipambana usiku
na mchana na kutukumbusha mara nyingi kuhusu kuwajali watumishi wa kada nyingine
wanaotusaidia kwenye kazi mbalimbali ofisini na kwa ujumla wake hukupenda kuona
mtumishi yoyote anaonewa” Amesema Prof. Nonga.
Prof. Nonga amebainisha kuwa watumishi wote wa Sekta ya Mifugo wataendelea kuenzi utaratibu wa kutunza thamani ya muda jambo ambalo lilisisitizwa mara zote na Prof. Ole Gabriel wakati wakati wa uongozi wake. “Lakini pia wakati wote ulisisitiza kufanya kazi kimkakati ikiwa ni pamoja na “kubrand” Wizara kupitia njia mbalimbali na kudumisha ushirikiano baina yetu na Taasisi mbalimbali” Amesema Prof. Nonga.
Prof. Elisante Ole Gabriel ametumikia nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) kwa kipindi cha miaka mitatu na moja ya kazi kubwa aliyoifanya wakati akitumikia nafasi hiyo ni kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Comments
Post a Comment