Na
Rhoda Simba, Dodoma.
ILI
kuvisaidia viwanda vya ndani viweze kuzalisha sukari kwa wingi Waziri wa Kilimo,Profesa Adolf Mkenda amesema katu hatotoa kibali
cha uagizaji wa sukari nchini kwa mtu yeyote.
Akiongea
leo Agosti 30,2021,wakati wa uzinduzi wa matokeo ya sensa ya kilimo, mifugo na
uvuvi ya mwaka 2019-2020 ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),Waziri
Mkenda amesema suala la uingizaji wa sukari nchini limejaa rushwa ambapo amedai
ni kama madawa ya kulevya kwani imekuwa ikiwanufaisha watu wachache.
Amesema
huku nyuma kuna baadhi ya Mawaziri waliondolewa sababu ya sakata la utoaji wa
vibali vya uingizaji wa sukari ambapo amedai Serikali ya awamu ya tano na sita
imejipanga kuhakikisha inavisaidia viwanda vya ndani.
Waziri
Mkenda amesema kwa sasa mwenye Mamlaka ya kutoa kibali cha uingizaji wa sukari
ni Waziri wa Kilimo ambaye ni yeye hivyo hatotoa kwa mtu yeyote lengo likiwa ni
kuvisaidia viwanda vya ndani.
“Bunge
ndio limepitisha kibali cha ukitaka kuagiza sukari lazima uwe ni mzalishaji wa
sukari na mwenye uwezo wa kuzlaisha tani 40,000 na hakuna ambaye ataagiza
sukari mpaka kuwe na pengo,kibali kitapita kwangu na hakitapita bora niachie
ngazi tunamnufaisha nani,wanaopeleka majungu wapeleke tu juzi nimefuatwa Uwanja
wa ndege,hatutoi kibali NG’O,”amesema.
Hata
hivyo amesema iwapo sheria ya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi
itabadilishwa atakuwa tayari kujiuzulu kwani itakuwa imewabeba watu wenye
fedha.
Kuhusiana
na bei ya mafuta kuwa juu,Waziri Mkenda amesema Wizara imeweka mikakati ya
kuhakikisha mbegu ya zao la Alizeti inapatikana kwa wingi.
Vilevile,
amesema Serikali imejipanga kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha mbolea
inapatikana kwa wingi.
Kuhusiana
na uzinduzi matokeo ya sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi ya mwaka 2019-2020,
Waziri Mkenda amesema sensa hiyo imewasaidia kufanya uchambuzi namna ya kufanya
kilimo na ufugaji bora ambapo amedai sekta ya mazao inachangia asilimia 15 ya
pato la Taifa.
Amesema
wanaojishughulisha na mazao ni ni asilimia 60 lakini katika pato la
Taifa wanachangia kwa asilimia 15 ambapo amedai haki hiyo inaonesha kwamba
watanzania wanaumaskini mkubwa hasa wa maeneo ya vijijini,uwiano wa sekta za
uchumi ni mbaya pamoja na tija ndogo katika sekta ya kilimo.
Kwa
upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa amesema lengo la sensa
hiyo ni kutoa taarifa katika uzalishaji wa mazao,idadi ya mifugo na
ufugaji wa samaki ambapo amedai wametumia mfumo wa kidigitali
kukusanya takwimu mbalimbali.
Amesema
wametumia shilingi bilioni 6 ukilinganisha na mwaka 2007-8 ambapo walitumia
shilingi bilioni 10 ambapo walitumia fedha nyingi katika makaratasi.
Dkt
Chuwa amesema wametumia mwezi mmoja kutangaza matokeo ya utafiti tofauti na miaka
ya nyuma ambapo walikuwa wakitumia miaka miwili hadi mitatu.
Naye,Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma,Jabir Shekimweri ameiomba Wizara ya Kilimo kufungua duka la
mbegu ambalo litawasaidia wakulima kuweza kununua mbegu bora kwani wengi
wamekuwa wakiuziwa mbegu feki.
Mwisho
Comments
Post a Comment