Na. Edward Kondela
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
amesema anamshukuru sana Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete kwa kuwa ndiye aliyemuibua katika uongozi mwaka 2013 kwa kumteua kwa
mara ya kwanza kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamadani na
Michezo.
Prof. Gabriel amebainisha hayo (30.08.2021) wakati akizungumza
na menejimeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika ofisi za wizara hiyo jijini
Dodoma, wakati alipofika kwa ajili ya kukabidhi ofisi aliyokuwa akihudumu
katika nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo.
Aidha, Prof. Gabriel amebainisha kuwa siku chache kabla ya Mhe.
Dkt. Kikwete kuondoka madarakani Mwezi Oktoba Mwaka 2015, alimteua kuwa Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamadani na Michezo hivyo hana budi kumshukuru
kwa kuwa alionesha imani kubwa kwake.
Pia, amesema anashukuru aliendelea kuaminiwa na Rais wa Awamu ya
Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya Katibu
Mkuu wizara tofauti na Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye
alimteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo
nafasi ambayo alikuwa akiendelea kuihudumu hadi alipomteua tena hivi karibuni
kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
“Namshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa
na imani nami katika nafasi hii mpya aliyoniteua ya kuwa Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, na kwamba nitafanya kazi kwa nguvu na weledi mkubwa kwa
kushirikiana na wenzangu kwa kuwa nina deni kubwa la kulipa kwa Mhe. Rais
Samia, lakini pia kufikia matarajio ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim
Juma na matarajio ya watanzania wote katika mhimili huu kwenye utendaji wa
haki.” Amesema
Prof. Gabriel
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya
mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), katika ofisi
za wizara hiyo ambapo Waziri Ndaki amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani kubwa na Prof. Gabriel kwa
kumteua kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kutoka katika nafasi aliyokuwa
akihudumu ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo.
Waziri Ndaki amesema uteuzi aliopata, Prof. Gabriel kusimamia mhimili
muhimu katika taifa hili kwenye masuala yanayohusu haki kwa watanzania na
kwamba jambo hilo ni kubwa kwa kuwa ni mhimili muhimu kwa taifa.
“Mimi nikupongeze kwa kuaminiwa kwa kiasi hicho, kwa
sababu ni kwa kiasi kikubwa kwa kweli lakini nichukue nafasi hii kukushukuru
kwa muda ambao tumefanya kazi pamoja.” Amesema Mhe. Ndaki.
Mhe. Ndaki amesema wakati Prof. Gabriel alipokuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi katika sekta ya mifugo amekuwa msaada mkubwa kwake katika
utendaji kazi na kwamba amekuwa akitoa maelekezo na usimamizi wa majukumu
mbalimbali ya wizara na kutengeneza timu ambayo inaelewa majukumu yake.
Ameongeza kuwa wakati wa uwepo wake katika wizara hiyo Prof.
Gabriel amekuwa ni mtu wa kujitolea na kufanya kazi muda wowote bila kujali
siku wala saa na kwamba watumishi wengi wa wizara wanaweza kufanya mambo
makubwa na wizara itaendelea kuhitaji ushirikiano wake wa karibu kwa ajili ya
kupata uzoefu kutoka kwake kwa yale aliyokuwa akisimamia wizarani hapo.
Awali mara baada ya kukabidhiwa nyaraka muhimu za ofisi ya
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoshughulika na Mifugo, Kaimu Katibu
Mkuu Bw. Amosy Zephania amemshukuru Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa
utumishi wake wa miaka mitatu katika wizara hiyo kwa kuwa amejenga msingi
mkubwa wizarani hapo.
Bw. Zephania amefafanua kuwa atahakikisha anasimamia misingi
iliyoachwa na Prof. Gabriel na kuhakikisha anaisimamia vyema sekta ya mifugo
ili iendelee kuleta tija kwa wananchi hususan wafugaji na kuzingatia yote
ambayo mtendaji mkuu huyo wa mahakama amewaachia yakiwemo ya kushirikiana kwa
viongozi na wafanyakazi wote kwa ujumla.
Mwisho.
Comments
Post a Comment