WANANCHI WATAKIWA KUPATA RAMANI ZINAZOTOLEWA NA WIZARA YA ARDHI

                        

Na. Munir Shemweta

 

Wakati Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yakiendelea katika viwanja vya Mwl. Nyerere Dar es Salaam wananchi wametakiwa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kujipatia Ramani za Tanzania na ile ya jiji la Dar es Salaam.

 

Afisa Upimaji Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Vicky Sonda akionesha ramani ya jiji la Dar es Salaama wakati wa  Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea viwanja vya Mwl. Nyerere barabara ya Kilwa Dar es Salaam

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia idara yake ya Upimaji na Ramani ndiyo yenye jukumu la kutoa Ramani ya Tanzania, mikoa pamoja na zile za wilaya kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kupima mipaka yote ikiwemo ya nchi kavu na majini.

Akizungumza katika maonesho ya Sabasaba tarehe 1 Julai 2021 mkoani Dar es Salaam Afisa Upimaji wa Wizara ya Ardhi, Vicky Sonda alisema, wananchi wanaotembelea Banda la Wizara mbali na huduma nyingine wataweza kujipatia Ramani za Tanzania pamoja na zile za jiji la Dar es Salaam.

Alisema, Ramani za jiji la Dar es Salaam zinazopatikana kwenye Banda la Wizara katika Maonesho ya Sabasaba zitawasaidia wananchi hasa wageni kujua maeneo mbalimbali ya jiji kwa haraka bila kulazimika kuuliza.

 

Wananchi wakipata huduma katika Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea viwanja vya Mwl. Nyerere barabara ya Kilwa Dar es Salaam

"Ramani za jiji la Dar es Salaam zinazopatikana hapa zitaweza kumsaidia mwananchi kutambua eneo analoenda kwa uharaka bila kuuliza" alisema Vicky.

Kwa mujibu wa Vicky, wananchi watakaotembelea Banda la Wizara pia watajua uhalali wa umiliki wa tanzania maeneo ya mipaka ya bahari kupitia ramani alizozieleza kuwa zinaonesha maeneo ya mipaka baina ya Tanzania na nchi nyingine.

Aidha, Afisa huyo Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam alisema kuwa, fursa nyingine wanayoweza kunufaika wananchi wanaotembelea banda la wizara ya Ardhi ni kufahamu uwepo wa kisiwa ndani ya kisiwa cha Mafia  kinachoitwa Bwejuu.

"Wananchi watakaotembelea Banda letu watapata fursa ya kufahamu uwepo kisiwa ndani ya kisiwa cha Mafia kinachoitwa Bwejuu na kisiwa hicho ni maarufu sana kwa shughuli za utalii" alisema Vicky.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kutoa huduma mbalimbali katika maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ikiwemo kutoa hati za papo hapo kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

 

Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biasahara (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Nyerere barabara ya Kilwa Dar es Salaam

Wananchi wakipata huduma katika Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea viwanja vya Mwl. Nyerere barabara ya Kilwa Dar es Salaam

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.