Na. Erick Mwanakulya, TARURA
Wananchi wa Kata ya Suguti na Kataryo zilizopo katika Halmashauri ya
Wilaya Musoma, mkoani Mara wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA), baada ya kutatuliwa kero yao ya muda mrefu kwa
kujengewa Daraja la chuma katika Mto Suguti uliopo barabara ya Wanyere Kataryo.
Wakizunguma katika mahojiano maalum, wananchi wa Kata ya Suguti walisema
kuwa hapo awali kulikuwa na daraja la miti ambalo lilikuwa linahatarisha
usalama wao hasa kipindi cha masika na kukatisha mawasiliano hivyo kushindwa
kufika Wanyere ili kuweza kupata mahitaji yao na huduma za kijamii kama shule,
hosptali na masoko.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa Daraja ili la Suguti sasa
kwenda Kataryo si kikwazo tena watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule hasa
katika kipindi cha masika, tulikuwa hatuwezi kwenda upande wa pili na kusubiri
maji yapungue hata siku tatu mpaka nne ndipo tuweze kwenda Wenyere kupata
huduma za kijamii, kwa kweli tunaishukuru sana Serikali”, alisema Ndg. John
Changulu mkazi wa Wanyere.
Bw. Moshi Maligesi ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Wanyere ametoa
shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Samia S. Hassan kwa
jitihada zake anazoendelea kuzifanya katika kuongeza bajeti ya Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini ili kuimarisha utendaji kazi wake wa kuboresha
miundombinu katika maeneo mbalimbali.
Muonekanao wa daraja la awali lililokuwa linatumiwa na wakazi wa Kata ya Suguti na Kataryo lililopo katika barabara ya Wenyere - Kataryo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara
“Eneo hili la Mto Suguti ilikuwa ni shida sana kuvuka kwenda upande wa
pili hasa katika kipindi cha masika watoto walishindwa kwenda shule na
wajawazito walishindwa pia kufika hospitalini kupata huduma, kwani mawasiliano
huwa yanakatika kabisa, ila kwa ujenzi huu wa daraja tunaishukuru sana TARURA.
Naye, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mhandisi Hussein
Abbas alisema kuwa ujenzi wa daraja la chuma la Saguti katika Mto Saguti
umegharimu shilingi milioni 80 lenye urefu wa Mita 24 ambapo ujenzi wa daraja
hilo umepewa kipaumbele kwani ni muhimu kwa wananchi wa Suguti na Kataryo
katika kupata mahitaji yao ya kila siku kwa kuwa wananchi hao wanategemea
kupata huduma katika Kijiji cha Wanyere.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo la Suguti ni sehemu ya mikakati ya
TARURA ya kuboresha huduma ya usafiri na usafirirshaji hasa kwa maeneo ya
pembezoni ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Wakala umejipanga kuhakikisha
unawafungulia huduma wananchi ili mahali maliposhindwa kufikika sasa
pafikike na hii ni baada ya Serikali kuongeza bajeti ya Wakala.
MWISHO
Comments
Post a Comment