Na. Revocatus Kassimba, SUMBAWANGA
Wanachi wa kijiji cha Ntendo Manispaa ya
Sumbawanga wameiomba serikali kusaidia kupatikana kwa soko la mazao yao ikiwemo
mahindi ili waweze kupata fedha za kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi
wa zahanati na madarasa ya shule.
Wametoa maombi hayo kwa nyakati tofauti wakati
wakiongea na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alipotembelea kijiji hicho
kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Ntendo B ambapo ilianza
kujengwa mwaka 2018.
“Kero tuliyonayo hapa Ntendo ni soko la mazao sasa
mahindi tunauza kwa bei ya chini ambapo sado
moja inauzwa shilingi 800. Mimi mwaka
huu nimepata gunia 40 na sasa nimeshindwa kuuza, yapo tu nyumbani. Serikali
itusaidie” alisema mkazi wa Ntendo James Zumba kwenye mkutano huo.
Eliza Kachele alisema kero nyingine ya kijiji cha
Ntendo ni mrundikanao wa wanafunzi kwenye shule ya msingi ambapo inasababisha
wanafunzi kutosoma vizuri hivyo ameitaka Serikali kutoa fedha kukamilisha shule
mpya ya msingi ya Ntendo B inayojengwa.
Akijibu hoja za wananchi wa kijiji cha Ntendo, Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwashukuru wananchi hao kwa kujitokeza
kwenye mkutano huo na kuwasilisha kero zao.
Mkirikiti aliwaeleza wanachi hao kuwa Serikali inaendelea
kutafuta ufumbuzi wa soko la mahindi ambapo amewaeleza kuwa mahindi bado
yanahitajika nje ya nchi hivyo endapo mfumo wa ushirika ukitumika unaweza
kusaidia upatikanji soko.
“Mzizi pekee wa kufanya mahindi yapate bei ni
kuacha kuuza kiholela . Ili tuuze mahindi vizuri tuna jukumu la kuimarisha
vyama vya ushirika viweze kutafuta soko la uhakika la mahindi ili mkulima apate
fursa ya soko. Mfumo wa kila mtu kutafuta soko la mahindi unasababisha wakulima
wanyonywe” alisema Mkirikiti.
Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi wananchi kufuata
ushauri uliotolewa na Serikali endapo wanapata soko la mahindi nje ya nchi
wasiwekewe vikwazo bali wasaidiwe kulifikia soko hilo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza
Manispaa ya Sumbawanga kuboresha mazingira ya soko la wananchi wa Ntendo kwa
kuliwekea miundombinu ikiwemo paa na vibanda ili waepukane na jua na mvua
ambayo ni kero kwa sasa.
Kuhusu ujenzi wa madarasa ya shule mpya ya Ntendo
B Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa ameagiza Manispaa ya Sumbawanga kukamilisha ujenzi
wake kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu ili kuwa na uhakika wa kupunguza msongamano
kwenye shule iliyopo .
Akizungumzia mkakati wa Halmashauri ya Manispaa ya
Sumbawanga, Jacob Mtalitinya alisema katika mwaka huu fedha 2021/22 wamepanga
kukamilisha jumla ya vyumba 72 vya madarasa kwa kutumia fedha za mapato ya
ndani ya ili kuwa na uhakika wa mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza
mwaka 2022.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa anaendelea na ziara ya
kikazi Manispaa ya Sumbawanga kuzungumza na wananchi na kukagua miradi ya
maendeleo.
Mwisho
Comments
Post a Comment