SERIKALI NA MKAKATI WA KUONDOA TATIZO LA USIKIVU WA RADIO IFIKAPO 2025

Na Mwandishi Wetu,Morogoro

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Dkt. Faustine Ndugulile amesema Wizara yake imejielekeza katika kumaliza kabisa tatizo la usikivu wa radio na simu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo ya pembezoni na mipakani mwa nchi ifikapo mwaka 2025.

 

Waziri wa  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe, Innocent Bashungwa wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo cha kurushia matangazo cha TBC Taifa na TBC FM kilichojengwa kwa ufadhili wa UCSAF. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC,Dkt. Ayub Rioba na wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba

Waziri Ndugulile ameyasema hayo katika uzinduzi wa kituo cha kurushia matangazo ya TBC Taifa na TBC FM kilichopo katika kijiji cha Sesenga, wilayani Morogoro, Mkoani Morogoro, kituo kilichojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa lengo la kuboresha usikivu wa radio katika eneo hilo na maeneo ya jirani ikiwemo eneo la kimkakati katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere.

Amesema hadi sasa asilimia 66 ya maeneo ya kijeografia nchini yanapata huduma ya mawasiliano lengo likiwa ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2025. Kwa upande mwingine amesema matumizi ya intanet kwa sasa ni asilimia 43 lengo ni kufikia asilimia 100 pia ifikapo 2025. Kuwa upande wa usikivu wa radio tayari Wizara kupitia UCSAF imetangaza zabuni ya kupeleka mawasiliano katika kata 190 zilizo maeneo ya mipakani. 

Ili kuboresha mawasiliano ya simu na huduma zingine za utangazji katika eneo hilo, Waziri Ndugulile ameiagiza UCSAF kufanya mazungumzo na makampuni ya simu pamoja na watoa huduma za utangazaji kutumia mnara huo mpya kuwekeza katika eneo hilo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano ya simu na utangazaji.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe, Innocent Bashungwa ameipongeza Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kutekeleza kwa vitendo  ilani ya CCM ya 2021-2025 kwa kuiwezesha TBC kupata vifaa vya kisasa vitakavyoisadia kupanua na kuboresha usikuvu wa radio za TBC nchi nzima.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya kudumu ya Miundombinu, Mhe. Innocent Karogenis amesema Kamati inazopongeza wizara hizo mbili kwa kushirikiana katika kuzingatia mapendekezo yanayotolewa na Kamati.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa, mfuko huo umetoa Sh450 milioni kujenga kituo hicho cha kurushia matangazo na ununuzi wa vifaa vya kisasa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Mfuko katika kuhakikisha mawasiliano, yakiwemo matangazo ya redio yanafika kwa watu wote nchini. 

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha kurushia matangazo utakuwa na manufaa kwa wanananchi wa maeneo hayo pamoja na maeneo mengine ikiwemo mbuga ya Selous kwa kuwa wataanza kupokea matangazo ya TBC Taifa na TBC FM.

 

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.