RC MKIRIKITI AAGIZA FORODHA KILANGAWANA SUMBAWANGA KUANZA KAZI

Na. Revocatus Kassimba, SUMBAWANGA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Joseph Mkirikiti ametatua mgogoro uliodumu kwa miaka 27 baina ya wananchi na   pori la akiba Uwanda ambapo wananchi wamekuwa wakizuiwa kupita kwenye pori la akiba la hifadhi wanapokwenda kuvua samaki  Ziwa Rukwa.

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Joseph Mkirikiti

Mkirikiti ametoa agizo hilo alipokuwa akiongea na mamia  ya vijana na wananchi wa  kijiji cha Kilangawana na Ilambo kata ya Kilangawana   ambapo ameiagiza Halmashauri ya Sumbawanga na hifadhi ya pori la akiba la Uwanda (TAWA) kuanzisha kituo cha forodha kwa ajili ya kukata vibali na ushuru kwenye kijiji hicho hatua itakayoondoa usumbufu wa watu.

"Kuanzia sasa awepo Afisa Uvuvi hapa Kilangawana atoe huduma ya forodha kwa wavuvi bila kikwazo, nataka TAWA msisumbue wananchi wenye vibali" alisema Mkirikiti

Kijiana Frank Solokoto wa kijiji cha Ilambo alisema kero ya ukosefu wa forodha inawafanya wasafiri umbali mrefu kilometa 40 hadi kijiji cha Legeza kufuata huduma ya forodha na pia imesababisha askari wa pori la akiba Uwanda kuwakamata na kunyang'anya pikipiki na kudaiwa rushwa.

"Mhe. Mkuu wa mkoa mwaka Jana nilikuwa natoka kuvua samaki nikapita njia inayokatiza kwenye hifadhi ya Uwanda nikakamatwa wakaninyang'anya pikipiki, baada ya kuwapa kiasi  wakaniachia ila wakabaki na pikipiki, kwa kuwa kazi yangu ni kuvua samaki nikatafuta pikipiki ingine ambayo nayo walinikamata nayo, pikipiki hizo zimeuzwa na mahakama, sina kazi hapa sina pesa hata mia ya matumizi naomba msaada wako mkuu!!." Alisema Frank.

Mkuu wa mkoa huyo baada ya kusikia kilio hicho alimuita Frank na kumpatia shilingi elfu kumi ya matumizi papo hapo huku wananchi wakishangilia kwenye mkutano wa hadhara.

Frank alimshukuru Mkuu wa mkoa na kukiri makosa ya kupita hifadhini kinyume cha Sheria na kuomba ili kuondoa tatizo la wananchi kukamatwa hifadhini serikali ifungue forodha ya Kilangawana.

"Mkuu wa mkoa ahsante sana, forodha ya Kilangawana ikifunguliwa tutaokoa mapato na kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kukamatwa na wahifadhi wa Uwanda, naomba forodha ifunguliwe ya Kilangawana." Alisema Frank.

Maombi hayo yalipata Baraka ya Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta ambaye alimueleza mkuu wa mkoa mkutanoni hapo kuwa hata halmashauri iliwahi kupokea malalamiko hayo na kuyawasilisha kwa maandishi katika ofisi ya maliasili lakini hawajajibu.

Mkuu huyo wa Mkoa yupo kwenye ziara ya kazi kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwemo kutoa elimu ya kujikinga na UVIKO-19 kwenye Halmashauri za mkoa wa Rukwa.

 

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.