Na. Netho C. Sichali
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, imezindua rasmi na
kuanza kutoa, huduma za kulaza wagonjwa na Upasuaji wa Dharula, katika Hospitali
ya Wilaya ya Nyasa iliyojengwa katika Kijiji cha Nangombo, Kata ya Kilosa
Wilayani Hapa.
Akizindua
Huduma hizo Mkuu wa Wilaya ya Nyasa kanali Laban Thomas, amewata watumishi na
wahudumu wa Afya Wilayani hapa kutoa
huduma bora kwa Wazee, na wananchi na
wanaofika kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya,
na kufanya kazi kwa bidii na
kufuata maadili ya kazi pamoja na viapo walivyokula.
Kanali laban amefafanua kuwa mara baada ya kuanza
kutoa huduma ya kulaza wagonjwa, na Upasuaji wa Dharula, ni mategemeo yake
kuwa, huduma zitaboreshwa, na wananchi watapata huduma bora
za afya, na Wazee watathaminiwa zaidi ili kuwaenzi, kwa kazi walizofanya
kipindi wakiwa vijana za kulijenga Taifa la Tanzania.
Ameongeza kuwa atafurahi zaidi atakapoona Wazee
wakipewa huduma bila kuwabagua, wala kuwasumbua, kwa kuwa nao wamechangia
huduma nyingi za kulijenga Taifa letu, na kuwataka watumishi, kutoa Huduma kwa
kufuata Sheria Taratibu na Kanuni kwa kuzingatia Viapo walipoapa.
“Ndugu wananchi wa Wilaya ya Nyasa na Watumishi wa
Afya, leo tukiwa tunafungua Huduma hizi
za Kulaza wagonjwa, ninawataka, kuwapa Huduma bora wazee ambao nimewaalika leo,
katika Zoezi hili ili waone
tunavyozindua huduma hizi, na ninawaagiza wazee hawa tunatakiwa kuwajali kwa
kuwapa huduma bora, kwa kuwa nao walishafanya kazi za kulijenga Taifa .Aidha
watumishi na Wahudumu wa Afya mnatakiwa kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa na
wateja kwa kuwa wagonjwa wanahitaji hata faraja kutoka kwa Mtoa Huduma za Afya”.
Amesema Kanali Thomas.
Awali akisoma Taarifa ya Uzinduzi wa Huduma za
kulaza wagojwa na Upasuaji wa Dharula, katika Hospitali ya Wilaya ya Nyasa,
Kaimu Mganga Mkuu Wilaya ya Nyasa, Bw.Sixbert Maseti Ndunguru amesema, mara
baada ya Uzinduzi huo, wamejipanga kuhakikisha kuwa, watatoa Huduma Bora kwa
Wananchi wa Wilaya ya Nyasa wapatao 140,000, na wananchi wa wilaya jirani za
Nchi ya Msumbiji, kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi kwa kutoa Huduma Za
dharula za upasuaji, kupunguza kasi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa huduma
elimu za afya na matibabu bora ya Ugonjwa wa kisukari , shinikizo la Damu,
kansa kwa kuanzisha kliniki za kila wiki.
Amezitaja huduma zingine ni Dawa muhimu na
Vitenganishi vya maabara kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kununua
Dawa,Vifaatiba na Vitendanishi kwa wakati.
Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Nyasa wameipongeza
Serikali kwa Kuwatatulia changamoto ya Huduma za kulazwa wagonjwa na Upasuaji
wa Dharula kwa kuwa awali Hudumahizi walikuwa wakisafiri Umbali Mrefu wa
Kilometa 150 kupata matibabu katika hospitali ya Peramiho na songea.
Halmashauri ya Nyasa imekamilisha majengo saba ya
awali ya Utawala, maabara, stoo ya dawa,mionzi,wodi ya wazazi,na jingo la
kufulia, njia za kuunganisha majengo,Ujenzi ambao umegharimu Tsh Bilioni 2.291,
na ujenzi wa Wodi ya Wanaume wanawake na watoto Unaendelea.Mradi huu wa Ujenzi wa
Hospitali ya Wilaya unatarajiwa kuwa na majengo 22 ambayo yatagharimu Tsh
Bilioni 7.5.
MWISHO
Comments
Post a Comment