Na. Rhoda Simba, Dodoma.
KAMISHINA Generali wa Jeshi la
Magereza, Suleiman Mzee amesema katika kupambana na kupunguza msongamano wa
mahabusu kwenye magereza hapa nchini, wameanzisha ujenzi wa Magereza kila
Wilaya .
Ameyasema hayo leo jijini hapa kwenye
kikao cha 44 cha bodi ya Taifa ya Parole Makao Makuu ya Jeshi la
Magereza Dodoma ambapo kikao hicho hufanyika kwa mwaka Mara nne ikiwa ni
mpango wake wa kila mwaka Katika utendaji kazi wake huku kukiwa na uwezekano
wa muda huo kupungua kutokana na Ukosefu wa Wafungwa wanaopendekezwa
katika kujadiliwa.
Meja Jenerali Suleiman Mzee, ambaye
pia ni Katibu wa Bodi ya Parole amesema, kutokana na Msongamano wa Wafungwa na
Mahabusu Magerezani, Jeshi la Magereza lipo kwenye mkakati wa kujenga Magereza
mapya kila Wilaya, na kuongeza Magereza ya Ngome, ambapo tayari Magereza Manne
yamesha jengewa Ngome na kwamba kutokana na Gonjwa la CORONA zinafuatwa kanuni
zinazotolewa na Serikali katika kuhakikisha ugonjwa huo hauingii Magerezani.
"Hiki ni kikao Cha 44 cha Bodi,
nashukuru kimeenda vizuri, hii ni njia moja wapo ya kupunguza Msongamano
Magerezani, Kama mnavyojua zipo njia nyingi ikiwemo ya Msamaha wa Raisi lakini
Jeshi pia tuna mkakati kuhakikisha tunajenga Magereza kila Wilaya, lengo sio
kuongeza watu bali ni kuwatawanya Wafungwa katika Magereza hayo, ili
wasirundikane katika Gereza moja". Alisema CGP Mzee.
" Bodi hii inatakiwa kukaa
Mara nne kwa Mwaka, lakini wakati mwingine hazitimii kutokana na ukosefu wa
Wafungwa wanaokidhi vigezo vya kusamehewa kupitia huduma hii, lakini wakiwepo
ndio Kama hivi tunakutana, na baada ya hapa, haya majina tuliyopendekeza
yatawasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwaajili ya kuwaachilia
rasmi". Aliongeza CGP Mzee
Awali akizungumza na wakati wa kikao
hicho Mwenyekiti wa Bodi hiyo Taifa Mh. Augustino Lyatonga Mrema amesema, lengo
la Bodi hiyo kukutana ni kuyapitia na kuyajadili Majalada ya Wafungwa
waliopendekezwa kuachiwa kupitia huduma hiyo na kisha kuyatolea mapendekezo
Majalada yaliyokidhi vigezo.
"Leo hapa tulikuwa na Majalada
ya Wafungwa 76, nashukuru wajumbe wamefanya kazi nzuri na tumefanikiwa
kupendekeza Wafungwa 70, na Wafungwa Sita pekee ndio hawajapendekezwa
kwakutokidhi vigezo vinavyohitajika". Amesema Mrema.
Aidha Mrema amesema kuwa, Magereza
yamekuwa na Msongamano mkubwa hasa wa Mahabusu, ambao hufikia 17000 hivyo
amelitaka Jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi kwa haraka ili Mahakama nayo
iweze kutoa haki kwa haraka, kwani idadi hiyo ya Mahabusu ni kubwa kuizidi
idadi ya Wafungwa, ukizingatia Mahabusu hawatumiki katika uzalishaji ndani ya
Magereza.
"Mahabusu wamefikia Elfu kumi na
Saba, ni idadi kubwa Sana hii, ukizingatia Mahabusu wanalelewa hawafanyi
uzalishaji wowote, ningeziomba taasisi Kama Polisi na Mahakama kufanya kazi zao
kwa haraka ili haki itolewe kwa wakati, itasaidia kupunguza Msongamano wa
Mahabusu Magerezani". Aliongeza Mrema.
Comments
Post a Comment