MWAMBE AWAONYA MAAFISA BIASHARA WANAOFUNGA MADUKA YA WAFANYABIASHARA

 

 


Na Sarah Mazengo, Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geofrey Mwambe, amewataka Maafisa Biashara nchini kuacha tabia ya kufunga maduka ya wafanyabiashara wanaodaiwa kwani kufanya hivyo ni kosa sawa na uhujumu uchumi.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua semina kwa Maafisa biashara wa mikoa iliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema kuwa vitendo vya Maafisa biashara kufunga maduka ya wafanyabiashara kutokana na kudaiwa mapato au kuisha kwa leseni siyo jambo la busara.

“Unakuta mtu anadaiwa fedha kiasi kidogo tuu labda leseni yake imeisha siku chache zilizopita lakini Afisa biashara anafunga duka na kufuli jambo hili ni sawa na ilivyo katika kosa la uhujumu uchumi” alisema Mwambe

Alisema kuwa badala ya maafisa biashara hao kufunga makufuli maduka ya wafanyabiashara watumie busara kwa kuwaita na kukaa nao meza moja ili kujadili namna bora ya kulipa madeni yao.

Wakati huohuo alisema ipo haja ya kufanyika mabadiliko katika usimamizi wa fedha za asilimia 10, zinazotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wakinamama, vijana na walemavu.

“Jambo hili mlisimamie na siyo Maafisa Maendeleo ya jamii kwani wao hawafahamu chochote kuhusu biashara bali wanachotakiwa kufanya ni kusajili vikundi na kuhakikisha vinapata mikopo”alisema Mwambe

Aidha alisema kuwa kutokana na kuwatumia maafisa maendeleo ya jamii kusimamia mikopo hiyo ya asilimia 10, kunaweza sababisha vikundi vingi kushindwa kupiga hatua kutoka na kukosa wataalamu wa masuala ya biashara.

Pia, aliwataka Maafisa biashara hao kuacha urasimu katika mikoa yao pindi wanapojitokeza wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali.

“Ili kuvutia wawekezaji tunahitaji kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuaandaa vibali kwa wakati lakini pia kuendeleza rasilimaliwatu”alisema

Kadhalika alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Tamisemi pamoja na Utumishi wapo katika mchakato wa kuunda idara ya bishara katika mikoa ili ijitegeme katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alisema hivi sasa Maafisa biashara hawana idara katika mikoa yao wapo chini ya idara ya fedha ambayo wanaisaidia kutafuta mapato.

“Lazima tujenge kada hii na iwe na uwezo wa kufanya kazi lazima tuwe na idara ya biashara hii ndiyo itatusadia kurahisisha masuala ya uwekezaji kwakua hatuna maafisa uwekezaji sasa lazima tuwageuze nyie ndiyo mfanye kazi hii” alisisitiza Mwambe

Hata hivyo akizungumza hapo awali Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania Dk. Maduhu Kazi, alisema kuwa lengo la kikao hicho cha siku mbili ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uwekezaji.

 

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.