JKCI YACHAGULIWA KUWA KITUO CHA MAFUNZO YA MAGONJWA YA MOYO

 




Na. Salome Majaliwa - JKCI

30/06/2021 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imechaguliwa kuwa kituo cha mafunzo cha magonjwa ya moyo katika mfumo wa umeme wa moyo kwa wataalamu wa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa kwa njia ya mtandao na wataalamu wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo  kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa magonjwa ya moyo, Dkt. Tatizo Waane alisema mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa wakati wa kambi maalum za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo zitakazokuwa zinafanyika katika Taasisi hiyo.

Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo alisema katika kambi hizo maalum za matibabu licha ya kutibu, wataalamu wanabadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo unaokwenda kwa haraka.

 “Katika kambi hizi huwa mafunzo yanafanyika kwa wataalamu waliopo katika Taasisi yetu pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) ambao wanapenda kujifunza matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo. Katika kambi zijazo mafunzo yatakuwa yanatolewa kwa njia ya mtandao ambapo wataalamu kutoka nchi mbalimbali watashiriki”, alisema Dkt. Waane.

Akizungumzia kuhusu kambi maalum ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo iliyomalizika hivi karibuni Dkt. Waane alisema walifanya matibabu kwa wagonjwa 10 ambao wawili kati yao walitoka nchini Burundi wote wanaendelea vizuri na wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Dkt. Waane alifafanua, “Matibabu haya yamefanyika katika mtambo wa Carto 3 System 3D & mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo ambao ulizinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katikati ya mwezi wa sita mwaka huu ambapo hadi sasa jumla ya wagonjwa 194 wamepata matibabu”,.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo  Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri  alisema mtambo huo wa  kisasa na wenye teknlologia ya hali ya juu licha ya kutumika katika kuokoa maisha ya watu wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo pia unasaidia  kutoa elimu kwa wataalamu.

“Mimi pamoja na wataalamu wenzangu kutoka nchini Misri kazi yetu ni  kutoa huduma ya kufanya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuokoa maisha ya watu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara”,alisema Prof.Mervat.

Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini Misri wanatoa  elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo ambapo madaktari wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.

Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ambaye ndiye msimamizi wa kambi hiyo Yona Gandye alisema wameweza kutoa matibabu kwa mgonjwa ambaye alikuwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ambapo moyo wake ulikuwa ukijaribu kufua umeme inashindikana katika hali ya kawaida na kuwa katika mtiririko wa hali ya juu (Atrial fibrillation), hali hii ikitokea mgonjwa anakuwa katika uhatarishi wa damu kuganda na kupelekea kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi.

“Matibabu haya yametolewa  kwa mara ya kwanza katika  nchi za Afrika Mashariki  na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ingawa mtambo kama huu umefungwa nchini Kenya lakini matibabu kama haya hayajawahi kutolewa”, alisema Dkt. Gandye ambaye pia ni mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo.

Alisema katika kambi ijayo ambayo itafanyika baada ya miezi miwili kutakuwa na mafunzo kwa njia ya mtandao ambayo  yataunganishwa  na hospitali ambazo  hazijaanza kutoa huduma ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo  ili madaktari waweze kupenda kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa ambayo itawasaidia  kutokusafiri nchi za mbali kwenda kutafuta matibabu ya aina hiyo.

Mwisho.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.