Na. Noelina Kimolo, DODOMA
SERIKALI mkoani Dodoma
imewahakikishia wazee kuwa itaendelea kusimamia sera ya wazee kwa lengo la
kuwahakikishia upatikanaji wa huduma bora kwa ustawi wa maisha yao kutokana na
mchango wao mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Khamis Mkanachi akiongea na Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma |
Hakikisho hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya
ya Kondoa, Khamis Mkanachi alipomuwakisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, katika hafla
fupi ya uzinduzi wa Baraza la Wazee la Mkoa wa Dodoma lililofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkanachi alisema kuwa serikali
kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 imeeleza kuwa wazee ni kundi
muhimu katika jamii na wanapaswa kutambuliwa na kupewa fursa ya kushiriki
katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku kwa manufaa ya watanzania wote. Vilevile,
inahakikisha wazee wanapata huduma zote muhimu ambazo zitawawezesha kushiriki
kwa ukamilifu katika Maisha kila siku. Hivyo, ustawi wa wazee ni wajibu wa
serikali, aliongeza.
“Serikali inaendelea kuwahudumia
wazee katika upande wa afya, lishe na huduma zote za msingi ili kukidhi
mahitaji ya mwanadamu huu ni wajibu wa msingi ambao serikali yetu imeuchukua”
alisema Mkanachi.
Akiongelea uongozi wa baraza la wazee
uliochaguliwa, alisema kuwa unawajibu wa kuwasaidia na kuwatetea wazee ili
waweze kusimamia haki na ustawi katika kupewa kipaumbele kwenye huduma
mbalimbali.
“Na utamaduni huo umekuwa ukiendelea
kila siku na ndio maana hata sisi tukaona ni muhimu kuwa na Baraza la Wazee
katika kuleta maendeleo ya taifa’’ alisema Linuma.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa
wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo alisema kuwa ni muhimu kwa wazee kujua haki zao
katika kufanya maamuzi ili kuleta maendeleo katika jamii.
“Sisi wazee tunayo mambo mengi ambayo
serikali tunahitaji mtusaidie. Wazee waliochaguliwa kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa
hawajui kazi yao na mipaka hivyo, tumeomba kupewa semina za mabaraza ya wazee
ili watambue wajibu wao katika kazi zao” alisema Mchungaji Mpolo.
Pia ameomba halmashauli ziwe zinatenga
bajeti za kuwawezesha wazee kutekeleza majukumu yao kuanzia ngazi za chini hadi
juu.
MWISHO
Comments
Post a Comment