WIZARA YA AFYA YAKAGUA MUONGOZO NA. 7 WA USHAURI WA WASAFIRI UWANJA WA NDEGE -KIA

Na. Catherine Sungura, WAMJW-Kilimanjaro

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, jana ametembelea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiwa ni kufuatilia utekelezaji wa muongozo namba 7 wa ushauri wa wasafiri wanaoingia nchini uliotolewa tarehe 4 Mei, 2021.



Katika muongozo huo moja ya maelekezo ni kufanya uchunguzi wa COVID-19 kwa kuwapima kipimo cha haraka (Rapid Test) wasafiri wote wanaoingia nchini, kwani kumekuwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa wananchi kuhusu zoezi hilo. Mojawapo ya malalamiko hayo ni abiria kuchelewa kumaliza hatua za huduma ya vipimo vya afya.

Mhe. Waziri amebaini kuwa watumishi wapo na wanafanya kazi zao vizuri wakiwemo maafisa afya, maabara na watumishi wa uwanja wa ndege. Waziri amewapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri wanaoifanya. Aidha, amewashukuru viongozi wa mkoa wa Kilimanjarao na Halmashauri ya Hai, Moshi kwa kutoa watumishi wa ziada ili kuongeza nguvu.

Amesema kuwa abiria kuchelewa kumaliza hatua za vipimo vya afya pia inachangiwa na baadhi yao kutojaza taarifa zao za hali yao ya afya kupitia mfumo wa kieletroniki wa afyamsafiri ambao unamtaka abiria kujaza taarifa zake ndani ya masaa 24 kabla ya kuingia nchini na hivyo kuwafanya wachelewe kuanza hatua ya uchunguzi wa awali (primary screening) na mwisho kufanya hatua zote za kulipia na kupima kuchelewa pia.

Aidha, ametoa wito kwa mashirika ya ndege na mamlaka ya viwanja vya ndege, usafiri wa ndege na wakala wa ndege, mabasi kushirikiana kutoa elimu ili taarifa hizo zijazwe mapema kabla ya kufika katika maeneo yetu ya viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote.

Kwa upande wa vipimo vya awali ameelekeza ufanyike utaratibu wa kuongeza idadi ya wapimaji kutoka watano hadi kufikia 8 na wakati huo uratibu ufanyike kuomba wahasibu kutoka wizara ya fedha kwa ajili ya kuratibu malipo kwa ushirikiano na banki husika na wataalamu wa afya wahusike na kuongeza nguvu ya kutoa huduma za afya.

Pia kwa kuzingatia kuelekea msimu wa wageni wengi wizara itashirikiana na wadau wake kuimarisha huduma za vipimo vya haraka huku ikiendelea kupokea maoni mbalimbali na kuyafanyia kazi. Vilevile, amesema wizara itaendelea kuboresha mfumo wa afyamsafiri ili uweze kurahisisha taratibu za kuwahudumia wasafiri kabla hawajaanza safari na kupunguza changamoto mbalimbali wanazolalamikia wakati wanapowasili nchini.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.