Na. Mwandishi Wetu, WAMJW, DODOMA
Wizara ya
Afya inatarajia kuja na mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito wote toka
wanapofika kliniki kwa mara ya kwanza hadi baada ya siku 42 za kujifungua.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima leo alipokutana
na wataalam wa afya katika kikaokazi cha maandalizi ya utengenezaji wa mfumo
huo.
“Nataka
muwe mnafuatilia taarifa za wajawazito na kujua maendeleo yao toka wanapofika
kituoni siku ya kwanza mpaka baada ya kujifungua kwa data za kila siku na kujua
kwa namna gani wajawazito au mama baada ya kujifungua ameweza kupata huduma
zetu na muweze kuchukua hatua pale mnapoona changamoto” amesema Dkt. Dorothy
Gwajima.
Waziri
Gwajima amesema kuwa ili kuweza kuwa na mfumo wenye ufanisi ni lazima
tusisitize matumizi sahihi ya takwimu na kuwataka wataalam wa afya katika kazi
zao kuhakikisha wanachukua takwimu zote zinazohitajika kwa ajili ya matuzimu
katika mfumo huo.
Waziri
Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali katika kupambana na vifo vya wajawazito
imefanya mambo mengi ikiwemo kuanzisha Kampeni maalum ya Jiongenze Tuwavushe
Salama iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kupunguza na
kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.
“Serikali
imejenga vituo vingi vya huduma ngazi zote na mwamko wa wajawazito
wanaojitokeza kuhudhuria kliniki umekuwa mkubwa” amesema Dkt. Dorothy Gwajima
na kuongezea kuwa bado elimu inahitajika kutolewa kwa ili wajawazito wafike
katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuanza kliniki mapema.
“Sasa hivi
mwitikio umeongezeka, wajawazito wanajitokeza na kujifungua katika vituo vya
kutolea huduma kati yao wengine wanafariki, lakini tukijadili kujua kwanini
amefariki na tukifuatilia wakati alipokuwa kliniki tunagundua hatukumfuatilia
vizuri, hiki ndio kitu tunachoimarisha ili ufuatiliaji uwe imara” amefafanua
Dkt. Dorothy Gwajima.
MWISHO

Comments
Post a Comment