WADAU WA PARETO WAKUBALIANA KUONGEZA UZALISHAJI HADI TANI 9000 IFIKAPO 2022/23

Na. Revocatus Kassimba, DODOMA

Tanzania imedhamiria kuendelea kuongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la pareto toka tani 3000 mwaka 2021 hadi kufikia malengo ya tani 9,000 kutokana na uwepo wa viwanda vitatu vya kuongeza thamani zao hilo.

Naibu Waziri Kilimo Mhe. Hussein Bashe akizungumza na wadau wa zao la pareto leo katika ukumbi wa Treasury Square jijini Dodoma ambapo ameeleza mikakati ya wizara na wadau kufikia uzalishaji wa tani 9,000 ifikapo mwaka 2022/23


Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma wakati wa kikao cha wadau wa zao la pareto toka mikoa sita nchini kilichoshirikisha viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri, makampuni ya pareto na wawakilishi wa wakulima.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwapongeza wadau kwa kuweka lengo hilo la kufikisha tani 9,000 za maua ya pareto ambapo viwanda vitatu vilivyopo sasa vitaweza kuinunua yote kulingana na uwezo wake.

Bashe alisema ili kufikia malengo hayo ya uzalishaji wizara kupitia Bodi ya Pareto na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) itawekeza kwenye utafiti wa mbegu bora za pareto na kuhakikisha zinapatikana kwa wingi na kugawiwa kwa wakulima nchini.

Sehemu ya wadau wa zao la pareto wakiwa kwenye kikao leo Jijini Dodoma ambapo wamekubaliana kuongeza ubora na uzalishaji wa zao hilo kufikia tani 9,000 msimu ujao endapo mbegu bora zitapatikana


“Tunahitaji mbegu bora za pareto tani 3 ili zitumike kuzalisha tani 9,000 za pareto baada ya mwaka mmoja ambapo viwanda viko tayari kuinunua toka kwa wakulima” alisisitiza Bashe.

Naibu Waziri huyo alizipongeza Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) ambayo itanunua tani 6,000 kwa mwaka huku kampuni ya TAN Extract Ltd ikihitaji tani 1,000 na kampuni ya PYTECH Ltd  ikihitaji tani 2,000 za maua ya pareto itakayozalishwa na wakulima msimu wa 2022/23.

Katika hatua nyingine Bashe alibainisha mikakati ya wizara kuhakikisha zao la pareto linakuwa na tija na uzalishaji wake unaongezeka zaidi ambapo alitaja mambo sita.

Kwanza kuongeza utafiti na uzalishaji wa mbegu bora tani 3 kupitia TARI, pili kuanzisha mfumo wa kilimo mkataba (Contract Farming), tatu kuanzisha mfumo wa ushirika kwa kuanzisha AMCOS za wakulima wa pareto.



Mkakati wa nne ni kuhamsisha Halmashauri kutenga mashamba vitalu (Block Farming) kisha kugawa kwa wakulima ambapo lengo kuanzia ekari 200, tano ni kusajili na kuwatambua wakulima wa pareto na sita wizara itaendelea na juhudi za kuondoa migogoro baina ya wanunuzi kwa kutenga kanda (Zone of production).

Kwa upande wake Mkulima bora wa zao la pareto Mzee Anangisye Mwankina kutoka Kata ya Ipelele Kijiji cha Makwaranga Tarafa ya Magoma wilaya ya Makete ametoa ombi kwa wizara ya Kilimo kuwashirikisha viongozi wa wilaya nchini kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakulima wa pareto ili ubora wa zao uongezeke hatua itakokuza bei.

Mwankina ambaye amekuwa mkulima bora wa pareto tangu mwaka 2014 hadi sasa ametoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kutembelea wakulima wa Makete hatua itakayoongeza ari ya Kilimo hicho.

“Ninalima ekari 3 ambapo kwa mwaka navuna kilo 800 na ubora wangu umefikia 1.8% lakini tatizo letu mabenki yanatukopesha kwa riba kubwa mno hatua inayotukwamisha. Tufikishie salamu kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aje atutembelee Makete” alisema Mzee Mwankina.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kushoto) ameziagiza halmashauri nchini kutenga maeneo maalum (Block Farming) ya kuanzia ekari 200 kwa ajili ya kuwagawia wakulima ili waongeze uzalishaji wa zao la pareto hatua itakayoongeza mapato ya ndani ya halmashauri hizo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Andrew Tsere


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini Lucas Ayo alisema uzalishaji wa zao la pareto umeongezeka toka tani 2,011 mwaka 2015/16 hadi kufikia tani 2,510 mwaka 2019/20 kati ya lengo la kuzalisha tani 3,000.

Aidha alibainisha kuwa tija imeongezeka toka wastani wa kilo 250 kwa ekari mwaka 2015/16 hadi kufikia kilo 270 kwa ekari mwaka 2019/20 huku wastani wa bei ya chini anayolipwa mkulima imepanda toka shilingi 1500 mwaka 2015/16 hadi shilingi 2,400 mwaka 2019/20 na shilingi 2,500 mwaka 2020/21 kwa kilo moja ya pareto.

Ayo alitaja mkakati wa Bodi ya Pareto katika mwaka 2021/22 ni kuongeza utafiti wa kina kuhusu matumizi mbalimbali ya bidhaa za pareto ikiwemo visumbufu vya mimea mashambani, majumbani na kwenye maghala ya mazao hatua itakayochochea kukuza kilimo na tija cha zao la pareto.

Naye   Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza alisema wakulima wa Mbeya vijijini wanaomba Wizara ifanye zao la pareto kuwa zao la kimkakati kwani ndilo linategemewa zaidi kimapato.

Mdau huyo alitoa wito kwa Wizara ya Kilimo ichukue hatua za haraka kuisaidia bodi ya pareto kifedha na watumishi ili isimamaie zao hili kwa ufanisi na kuwa sasa bodi haifanyi vizuri kwenye usimamizi wa zao hatua inayopelekea wakulima wakate tama.

“Zao la pareto kwa muda mrefu limekosa ushindani hatua inayosababisha liwe na bei ndogo, hivyo wizara ihamasishe wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuongeza thamnai zao la pareto” alisema Njeza.

Kuhusu suala la kutenga maeneo ya kilimo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga alisema wamelenga kuongeza eneo la uzalishaji pareto toka ekari 40 za sasa hadi kufikia ekari 100 kwa kutumia Block Farming hatua itakayokuza uzalishaji ambapo msimu huu wamezalisha tani 4.3 za pareto.

Zao la pareto kwa sasa linalimwa kwenye mikoa ya sita ya Arusha, Manyara, Songwe, Njombe na Iringa ambapo Bodi imefanikiwa hadi kufikia Februari 2021 imesajili wakulima 10,586 kwenye mfumo wake wa utambuzi na huduma kwa wakulima.

 

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.