Waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo waahidi kuendelea kushirikiana na JKCI ili wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wapate dawa kwa wakati
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na waagizaji
na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano
baina yao ambao ulijadili changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua ikiwa
ni kuboresha upatikana wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Mkutano
huo ulifanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalum – Dar es
Salaam
25/05/2021 Uongozi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umekutana na waagizaji na wasambazaji wa dawa
za binadamu za moyo ili kujua changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua
ikiwa ni kuboresha upatikana wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo.
Kikao hicho cha wadau hao
kilifanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
ambapo wawakilishi zaidi ya 30 kutoka kampuni mbalimbali za dawa walihudhuria.
Akizungumza mara baada ya
kumalizika kwa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema lengo la kukutana na wadau
hao ilikuwa ni kuangalia changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Prof.Janabi ambaye pia ni
daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema ukikosa dawa za moyo unahatarisha
maisha ya mgonjwa hivyo basi kujenga uhusiano na wadau hao ni jambo la
muhimu. Siku za nyuma mawasiliano yao yalikuwa kwa kupitia mitandao
(barua pepe), simu na sio kuonana uso kwa uso kama ilivyotokea katika kikao hicho
wameweza kufahamiana jambo ambalo litawasaidia katika utendaji wao
wa kazi wa kila siku.
“Kulikuwa na changamoto za
mawasiliano, kutokufuatwa kwa taratibu za kuagiza dawa, kutokufahamu maoteo ya
dawa sawa sawa, kutoletwa dawa zote kamili kama zilivyoagizwa haya yote
tumeyazungumzia na kupata utatuzi. Katika Taasisi yetu hatukuwa na matatizo
ya upatikanaji wa dawa kwa asilimia 85, ninaamini baada ya kikao hiki tutakuwa
na uhakika wa upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100 na mgonjwa atapata dawa zote
alizoandikiwa na daktari”.
“Tutakuwa na maoteo ya
dawa sahihi zaidi baada ya mazungumzo yetu, kwani ukiwa na dawa za kutosha kwa
kipindi cha miezi 3 hadi 4 na ikifika katikati ya miezi miwili ukaagiza zingine
una uhakika wa kuwa na dawa za kutosha muda wote. Haya ni baadhi ya mambo
ambayo tumekubaliana”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema
tangu kuanzisha kwa Taasisi hiyo sasa ni mwaka wa sita na hii ni mara ya kwanza
kuwa na mkutano na wasambazaji wa dawa. Wamekubaliana kadri hali itakavyoruhusu
watakutana angalau mara moja kwa mwaka.
“Sisi tunanunua dawa zetu kutoka
Bohari ya Dawa (MSD) kama MSD hawana baadhi ya dawa tunazohitaji tunatangaza
zabuni hivyo basi hawa waigizaji na wasambazaji wa dawa ni wadau muhimu
kwetu”, alisisitiza Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo
cha Ununuzi na Ugavi cha Taasisi hiyo Bunare Danieli aliwajulisha washiriki
kuwa ununuzi wa umma unaongozwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya
mwaka 2011 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake ya mwaka
2016. Hivyo, aliwaasa wajumbe hao kuifahamu vyema sheria hiyo na kuizingatia
wakati wote wanaposhiriki katika zabuni za umma na utekelezaji wa mikataba.
Aidha, aliwakumbusha kushiriki
mafunzo mbalimbali ya Sheria ya Ununuzi wa Umma yanayoandaliwa na taasisi
zilizothibitishwa kutoa mafunzo hayo hapa nchini.
Bunare pia aliwakumbusha watoa
huduma hao kuwa kuanzia Januari, 2020 Ununuzi wa Umma ulianza
kufanyika kupitia Mfumo wa Kielektroniki (Tanzania eLectronic
Procurement System – TANePS). Mfumo huo una lengo la
kuongeza ufanisi na uwazi katika ununuzi wa umma.
“Changamoto kadhaa
zinazotukabili wakati wa utekelezaji wa mikataba ya ununuzi ni pamoja na
ucheleweshaji wa bidhaa tofauti na muda ulioainishwa kwenye mkataba hali
inayosababisha Taasisi kukosa dawa na malipo kwa wazabuni kuchelewa, baadhi ya
wazabuni wanawasilisha mahitaji nusu nusu badala ya kuwasilisha kwa pamoja na
pia wazabuni wamekuwa wakichanganya oda zaidi ya moja kwenye hati moja ya madai
bila kutoa maelezo yanayojitosheleza”, alifafanua Bunare.
Nao waingizaji na
wasambazaji wa dawa walishukuru kwa mkutano huo ambao umeonesha ni jinsi gani
Taasisi hiyo ina nia ya kufanya nao kazi na kuhakikisha dawa zinapatikana
kwa wakati sahihi na kuziomba Taasisi zingine kuiga mfano huo.
Wazabuni wengi walionesha nia ya
kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kurekebisha
kasoro zilizoainishwa kwenye kikao hicho kwa lengo la kuhakikisha wao pia
wanakuwa sehemu ya mafanikio ya Taasisi hiyo.
Emmanuel Kasembe mwakilishi
kutoka kampuni ya Laborex Tanzania Ltd alisema kuitishwa kwa mkutano huo
kunaonesha ni jinsi gani Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejipanga
kuboresha huduma za matibabu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa zinapatikana
kwa wakati sahihi
“Changamoto kubwa tuliyokuwa
tunakutana nayo ni jinsi ambavyo tenda ilikuwa inatangazwa kwa muda mfupi na
utunzaji wetu wa kumbukumbu. Katika mkutano huu maelezo ya kina
yametolewa ya jinsi ya kukabiliana na changamoto hizi na ninaamini tutakuwa na
matokeo bora zaidi katika utendaji wetu wa kazi”, alisema Kasembe.
“Mkutano huu umesaidia kujenga
na kuimarisha uhusiano kati yetu na JKCI. Ninaomba uendelee kuwepo kwani
tumeweza kuzifahamu changamoto zinazowakabili JKCI nasi pia tumesema changamoto
zetu na kufikia muafaka. Hii itatusaidia kuimarisha huduma za usambazaji wa
dawa tunazozitoa siyo tu JKCI hata katika maeneo mengine”, alisema Jackline
Mally kutoka Horizon Pharmacy Ltd.
“Kitu kizuri kwa Taasisi hii
wanalipa madai yetu kwa wakati ndio maana leo unatuona tupo hapa makampuni
zaidi ya 30 lakini hamna mwenye kuidai Taasisi hii”, alipongeza Rupesh Pillai
Mkurugenzi Mtendaji wa Philips Pharmaceutical (T) Ltd.
Mwisho
Comments
Post a Comment