Na Mwandishi Wetu,Kongwa.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa Dk Omary Nkullo, amewataka wataalamu wa majengo kuhakikisha wanawaeka miundombinu rafiki itakayo wawezesha watu wenye ulemavu kupata huduma stahili kama ilivyo kwa wengine wasio na ulemavu.
Dk Nkullo amesema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja
kwa watumishi wa vituo vya afya na zahanati kutoka kata 5 za wilaya hiyo juu ya
upatikanaji wa huduma jumuishi za afya kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika
Kongwa.
Alisema kuwa majengo mengi yaliyojengwa miaka ya nyuma wilayani
humo hayana miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu suala ambalo linaloonyesha
bado kuna unyanyapaa na ubaguzi kwa upande wao.
“Hata hapa ofisini kwangu jengo hili naona lilisaulika wataalam
hawakuweka miundombinu rafiki ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kuingia kwa
urahisi hapa,cha kusikitisha hata huko kwenye vyoo havipo vinavyoweza kutumia
na ndugu zetu hao huu ni unyanyapaa na tena ni ubaguzi”alisema.
Hata hivyo amewataka wahudumu wa afya kuonyesha upendo kwa
vitendo kwa watu wenye ulemavu wanapo wahudumia kulingana na aina ya
ulemavu badala ya kuwanyanyapaa na kuwabagua.
Kwa upande wake Katibu wa Mkoa wa wa Dodoma Shirikisho la watu
wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Justust Ng’wantalima alisema kuwa unyanyapaa na
ubaguzi bado unawakatisha tamaa pindi wanapougua na kushindwa kupata huduma ya
kiafya.
“Pamoja na sababu zingine za kiuchumi,kitaasisi na kijamii
zinazowakabila watu wenye ulemavu,unawakatisha tamaa na kufikia hatua ya
kuficha hali zao pale wanapougua na kufikia hatua ya kuacha kutafuta
matibabu”alisema”alisema.
Naye Mtabibu wa afya Zahanati ya Mautya Kongwa Suzana
Petro,ameiomba serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wahudumu wa afya na zahanati
vilivyopo vijijini ili waweze kuwahudumia ipasavyo kulingana na ulemavu
alionao.
Mwisho.
Comments
Post a Comment