Na. Omary Mtamike, DODOMA
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Abdallah ulega ameliagiza Dawati la Sekta binafsi lililopo Wizarani hapo
kushughulikia haraka mchakato wa upatikanaji wa huduma ya bima kwa
wafugaji na wavuvi ili waweze kutekeleza kwa tija shughuli zao.
Ulega ameyasema hayo wikiendi hii wakati akipokea taarifa ya mafanikio ya Dawati hilo tangu kuundwa kwake ambapo alibainisha kuwa wapo wanunuzi wakubwa wa mazao ya mifugo na uvuvi ambao huwa hawalipi papo kwa hapo jambo ambalo mara nyingi huwafanya wafugaji na wavuvi kushindwa kufanya biashara kutokana na ukosefu wa mtaji.
“Msimu wa sikukuu ya Eid ya kuchinja
(Eid-El-Haji) mimi ninamfahamu mtu mmoja kutoka uarabuni ambaye huwa anachinja
hadi ng’ombe 15,000 na huwa ananunua kwa wafugaji wetu hapa nchini lakini
changamoto kubwa ni kwamba wafanyabiashara wengi hasa hawa wa kutoka nchi za kiarabu
hawalipi papo kwa hapo hivyo kwa wafanyabiashara wetu wa ndani inakuwa ngumu
kufanya nao biashara kwa sababu hawana mitaji mikubwa kiasi hicho na bahati
mbaya hawakopesheki hivyo ni lazima mazungumzo na Shirika letu la Bima yafike
mwisho ili hatimaye sasa tuzialike taasisi za fedha ziweze kuwawezesha
wafugaji na wavuvi wetu hapa nchini ” Aliongeza Ulega.
Kwa Upande mwingine Ulega ameiagiza
Idara ya Uzalishaji na Masoko kwa kushirikiana na Dawati la sekta binafsi
kuongeza wataalam wa utafiti na ubunifu wa masoko ili waweze kurahisisha
upatikanaji wa mahitaji ya soko, changamoto za huduma ambazo wadau wa sekta za
mifugo na uvuvi wanakumbana nazo, hali ya soko na mabadiliko ya huduma
ambayo inahitajika sokoni.
“Hawa wataalam wanaweza kupata “link”
na Ofisi nyingine za Serikali kama kituo cha uwekezaji na Wizara ya Viwanda na
Biashara lengo likiwa ni kutujulisha na kutushauri kipi kinapungua na kipi
kinazidi ili kila mara na kuangalia wadau wanasemaje kisha anatupa ushauri ili
sisi kama viongozi tufanye maamuzi sahihi na kwa wakati sahihi” Alisisitiza
Ulega.
Kwa upande wake Mtaalam wa benki
kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Zakayo Mphuru amesema kuwa
kabla ya kuanzishwa kwa Dawati la Sekta binafsi mikopo kwa upande wa sekta za
Mifugo na Uvuvi ilikuwa chini sana lakini hivi sasa mfumo wa uzalishaji wa
sekta hizo unazivutia taasisi za fedha kuwekeza fedha zaidi.
“Benki ya kilimo bado tuna mikopo
mingi na nimeshamkabidhi Msimamizi wa Dawati mikopo ambayo ipo kwenye ngazi ya
mapitio hivyo tunaomba Wizara itusaidie ili kuboresha upande wa Utawala hasa
usimamizi wa upande wa kutunza kumbukumbu za vyama ili benki iwe na uhakika
kwamba hela inapotoka lazima irudi ili ikawasaidie na watanzania wengine”
Alisema Mphuru.
Naye Afisa miradi mwandamizi kutoka
Taasisi ya utafiti,ushauri na maendeleo (DALBERG) Jackson Mahenge amesema kuwa
uwepo wa Dawati la sekta binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi umerahisisha
kwa kiwango kikubwa ufanyaji kazi wa Taasisi yao jambo ambalo limewapa shauku
ya kutamani kuona Wizara nyingine zikiwa na Dawati hilo.
“Tumefanya kazi na Wizara tofauti
lakini tumeanza kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la
Sekta binafsi tangu mwaka 2018 na nikiri wazi kuwa tangu tuanze ushirikiano
wetu tumepata fursa ya kufanya kazi na wadau tofauti jambo ambalo
linafanya tuanze kuona yale mabadiliko ambayo tumekusudia katika sekta za
Mifugo na Uvuvi “ Alihitimisha Mahenge.
Tangu kuanzishwa kwa Dawati la Sekta
binafsi ndani ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wafugaji na wavuvi wameweza kunufaika
kupitia mikopo mbalimbali ya fedha na nyenzo zinazowasaidia kutekeleza majukumu
yao kwa tija.
Comments
Post a Comment