ASKARI 3 WASIMAMISHWA KAZI UHAMIAJI

Na. Saleh Ramadhani, DODOMA

 

IDARA ya Uhamiaji imewasimamisha kazi askari watatu wa jeshi hilo ili kupisha uchunguzi kwa tuhuma za kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao.

 

Dkt. Anna Makakala

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala amebainisha kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na video fupi iliyokuwa ikisambaa mtandaoni ikiwaonyesha askari hao wakitumia nguvu kumkamata Alex Kyai ambaye ni mtuhumiwa wa makosa ya kiuhamiaji.

 

“Idara ya uhamiaji inakili kutokea kwatukio hilo na pia inalaani kitendo kilichofanywa na askari hao kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao hata hivyo idara ya uhamiaji tayari imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari hao ikiwemo kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao,” amesema.

 

Kamishna Jenerali huyo alibainisha kuwa tukio hilo lilitokea Mei 27 mwaka huu katika ofisi ya uhamiaji kurasini jijini Dar es Salam ambapo mtuhumiwa huyo alifika ofisini hapo na mteja wa paspoti za uhamiaji ambaye alimtambulisha kama mke wake.

 

Dkt. makakala amesema baada ya mahojiano ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kuwalaghai na kupokea fedha kutoka kwa wateja mbalimbali ili aweze kuwapatia  pasipoti haraka haraka.

 

“Hata hivyo tumebaini kuwa na matukio ya aina hiyo mengi ikiwemo kujitambulisha kama mtumishi wa Taasisi nyeti ikiwemo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili aweze kujipatia fedha kutokakwa watu mbalimbali wenye shida zinazofanana na taasisi hiyo,

 

“Mtuhumiwa huyo bado anaendelea kuhojiwa ili kujidhilisha zaidi kwani amekuwa na matukio ya kulaghai mengi na kwa muda mrefu”ameeleza

 

Kamishna Jenerali Dkt. Anna aliwataka wananchi wanaotaka huduma za uhamiaji kufika kwenye ofisi ili kuepusha utapeli ambao unaweza kujitokeza dhidi yao.

 

Alisisitiza kuwa idara ya uhamiaji itaendelea kutoa huduma zake kwa weredi, uwazi na bila kutumia mtu kati na kuwataka wananchi kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo vya kilaghai.

 

“Natoa onyo kwa mtu yoyote ambaye atajaribu kujifanya kuwa yeye ni afisa uhamiaji au afisa yoyote wa serikali ili kumsaidia mtu mwingine kwa maslahi yake binafsi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria” ameeleza.

 

Idara ya Uhamiaji inaendelea kuomba kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa Taarifa za watu wanaofanya vitendo vya aina hii.

 

 

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.